MBUNGE wa Rabai William Kamoti alifariki Jumapili usiku baada ya gari lake kugongwa na lori eneo la Mnarani, Kaunti ya Kilifi.
Mkuu wa polisi Kilifi Kaskazini Jonathan Koech alisema ajali ilitokea eneo hatari la Komaza katika barabara kuu ya Kilifi-Mombasa.
Wakazi walioshuhudia ajali hiyo walisema gari la mbunge huyo liligongwa na lori saa tatu na dakika 40 usiku. Dereva wake aliyepata majeraha amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Kilifi. Mwili wa mbunge huyo umehifadhiwa katika mochari ya hospitali hiyo.
Gavana wa Kilifi Amason Kingi amemtunuka sifa marehemu akimtaja kama kiongozi aliyejitolea na mchapakazi.
“Bw Kamoti atakumbukwa kwa sifa ya uongozi usio na vurugu uliomfanya awe kipenzi cha wengi katika eneobunge lake. Hili lilisaidia atomize mengi kwa wakazi wa Rabai. Kama kaunti, tumepoteza kiongozi mzuri,” akasema Gavana Kingi.
Kwa upande wake Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire alikumbuka jinsi walivyokuwa naye pamoja wakati wa kupeleka stakabadhi zao kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
“Bw Kamoti alikuwa miongoni mwa viongozi shupavu wa ODM katika Kaunti ya Kilifi hivyo ni pigo,” akasema Bw Mwambire.
Kindiki ahimizwa akubali uwaziri Ruto akishinda urais Agosti