RAIS Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wananchi wa Kigamboni cha viwango vya tozo wanazotozwa katika matumizi ya Daraja la Nyerere na kuamuru tozo hizo zishushwe.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi Godfrey Kasekenya jana alisema lengo la kushushwa kwa tozo hizo ni kuwapunguzia wananchi wa Kigamboni gharama, kutoa nafasi ya njia mbadala kwa wananchi wa Kigamboni na kupunguza msongamano wa watu kwa vivuko vya Kigamboni na Magogoni.
“Tozo zimeshushwa ili kuwapa wananchi wa Kigamboni njia mbadala pamoja na gharama, magari mengi yalikuwa hayatumiki kwa sababu ya gharama hivyo serikali imeona ipunguze bei na kumwezesha mwananchi kulipa kwa safari moja, kwa siku, kwa wiki au mwa mwezi,” alisema Kasekenya.
Awali taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge Jimbo la Kigamboni ilieleza kuwa mwananchi atakayelipia tozo ya siku ataweza kuvuka kwa idadi yoyote ya safari ndani ya siku husika na kwamba tozo mpya zilianza kutumika 20 Mei mwaka huu.
Taarifa ilieleza kuwa nauli za wiki na mwezi zitachelewa kuanza kutokana na kazi inayoendelea ya kurekebisha mifumo.
Tozo za bodaboda itakuwa Tsh 300 kwa tripu, 500 kwa siku, 2000 kwa wiki na 5000 kwa mwezi wakati bajaji kwa tripu itakuwa Tsh 500, 3000 kwa siku, 10,000 kwa wiki na 20,000 kwa mwezi.
Kwa upande wa magari madogo, tozo zake zitakuwa Tsh 1500 kwa tripu, 2500 kwa siku, 12,000 kwa wiki na 35,000 kwa mwezi.
“Kipekee namshukuru sana Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wana Kigamboni na kuagiza suala hili kufanyiwa kazi. Nawashukuru Mawaziri Waheshimiwa Profesa Makame Mbarawa na Profesa Joyce Ndalichako kwa usikivu na ushirikiano wao,” ilisema sehemu ya taarifa hiyto.
Ofisi ya Mbunge pia iliwashukuru makatibu wakuu, Aisha Amour na Profesa Jamal Katundu na Mtendaji Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na menejimenti yake kwa kulishughulikia suala hilo kwa uzito unaostahili.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ingawa wameishukuru serikali kilio cha wananchi wa Kigamboni ni kuondolewa kabisa kwa tozo katika Daraja la Nyerere.