Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amethibitisha taarifa za klabu hiyo kutozwa faini ya Shilingi Milioni 23.25 sawa na Dola 10,000, kwa kosa la kuwasha moto katika eneo la kuchezea mpira katika dimba la Orlando Pirates Afrika Kusini mwezi April.
CAF wameitoza faini Simba SC kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Uongozi wa Chama cha Soka nchini Afrika Kusini ‘SAFA’ siku moja baada ya mchezo wa mkondo wa pili wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Ahmed amesema taarifa hizo ni kweli, na klabu ya Simba SC inajutia kwa kosa hilo, hivyo imejifunza kutokana na makosa walioyafanya wakiwa ugenini.
Amesema tukio hilo limeharibu Taswira ya klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, lakini hawana budi kukubaliana na hali halisi, ili kupisha maisha mengine yaendelee ndani ya klabu Simba SC.
“Ukweli ni kwamba tukio lile lilichafua Taswira ambayo Simba tumeijenga kwa muda mrefu. Yote kwa yote inaangukia kwenye eneo la Bahati mbaya. Tumejifunza pakubwa na kwa wote waliokwazika tunawaomba msamaha na Maisha yaendelee.” amesema Ahmed Ally
Katika mchezo dhidi ya Olrando Pirates ambao ulishuhudia tukio hilo la kuwashwa moto eneo la katikati ya Uwanja, Simba SC ilitolewa kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati 4-3, baada ya kufungwa bao 1-0 ndani ya dakika 90.
Simba SC ilishinda bao 1-0 katika mchezo wa Mkondo wa kwanza uliounguruma jijini Dar es salaam, hivyo matokeo ya jumla kabla ya sheria ya kupiga mikwaju ya penati kutumika yalikua 1-1.