Wakati mshike mshike wa Ligi Kuu Tanzania bara ukiendelea kurindima nchini, imeripotiwa kuwa kumekuwa na udhaifu mkubwa wa kiushindani hali inayohatarisha ubora uliokuwepo kwa misimu kadhaa iliyopita.
Hayo yanafuatia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally kuandika kwenye mitandao yake ya kijamii akihoji kuwa iweje hadi sasa takribani timu 14 zigombanie kutokushuka daraja huku ikiwa tayari raundi 22 zimeshachezwa.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Ahmed Ally ameandika ''Kati ya timu 16, timu 14 zinaweza kushuka daraja, hii sio aina ya Ligi tunayoihitaji haiwezekani timu nyingi zigombanie kushindwa.
Ligi yenye ushindani ni ile ambayo timu nyingi zinagombania ubingwa, lakini msimu huu timu nyingi dhaifu, tupo raundi ya 22 lakini ni timu tatu tu zimefikisha alama 30+.
Msimu uliopita hadi kufikia raundi ya 22 japo timu zilikuwa nyingi lakini timu 7 zilikua na alama zaidi ya 30,hii ni hatari kwa sababu bingwa anaweza kupatikana kwa kufunga wadhaifu wengi.
Najua utauliza kwanini na wewe usiwafunge hao dhaifu wengi ili uwe bingwa, ukweli ni kwamba katika hizo mechi zetu dhidi ya timu dhaifu nasi tulifanya udhaifu.''Ahmed Ally Afisa Habari wa Simba.