Mbeya. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema suluhisho la umasiki wa Tanzania ni kupatikana kwa Katiba mpya.
Lissu anayeishi nchini Ubeligiji ameyasema haya alipokuwa akihutubia la kongamano la Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) lililofanyika katika mji wa Mbalizi jijini Mbeya, akisema kuna mfumo usiojali masilahi ya wananchi.
Akizungumzia masilahi ya wafanyakazi, Lissu amehoji sababu ya Rais Samia kutoweka wazi nyongeza ya mshahara akiishia kusema 'jambo lipo.’
"Tujiulize, Kenya iliyoweka watu lockdown imewezaje kuongeza asilimia 12 ya mshahara ilhali Tanzania ambao hakuna mtu aliyefungiwa ndani ikashindwa kuongeza mshahara?” amehoji Lissu.
Akizungumzia kurejea kwake nchini, Lissu amesema amesema muda si mrefu atawasili nchini, huku akieleza kuwa anachotaka akifika ni kufanya mikutano ya hadhara lakini kuhakikishiwa usalama wake kwani hakuna asiyejua jinsi alivyoondoka.
"Wana Mbeya na Watanzania kwa ujumla kaeni tayari narejea ndani ya wiki na siyo tena miaka, japokuwa lazima tushauriane kati yangu na nyinyi na viongozi ili kujua mazingira kama ni salama.
“Nikija nataka tufanye mikutano ya hadhara na siyo kujificha. Tutakutana hivi karibuni na siyo miaka tena," amesema Lissu huku akishangiliwa na wafuasi wake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Pambalu amesema amesikitishwa na kauli ya raisi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kuchukua muda mwingi kupongeza juhudi za Serikali badala ya kueleza kilio cha wafanyakazi.
Mwananchi