UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Muda wa kuteta na Yanga baada ya ubingwa wao



 
UNAHITAJA moyo mgumu wa Adolf Hitler kuamini kwamba Yanga hawatakuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Kwamba Yanga watashindwa kushinda mechi moja katika nne zilizobaki? Kwamba Yanga watashindwa kupata sare tatu katika mechi zilizobaki?

Kwamba Simba hawatadondosha alama katika mechi tano zilizobaki? Labda hili la Simba linawezekana, lakini hayo mawili ya mwanzo hayawezekani. Licha ya maajabu yote ya mpira, Yanga hawawezi kukosa ubingwa mwaka huu.

Njia pekee ya kuwanyima ubingwa kwa sasa ni kusimamisha ligi au dunia kufika mwisho. Unahitaji kuwa na mwili wa shetani unaoweza kuishi katika moto wa jehanamu ili ukubali kwamba Yanga hatakuwa bingwa msimu huu. Labda yatokee majabu makubwa yatakayonifanya nimeze maneno yangu.

Yatakapotokea hayo maajabu nitakuja hapa kuomba msamaha. Ni kweli Yanga watakuwa mabingwa lakini baada ya furaha za ubingwa kwa shabiki wa Yanga kichwani linakuja swali, kipi kinafuata?


 
Baada ya ubingwa wa msimu huu nini kinafuata kwa msimu ujao? Baada ya kuwa wanyonge kwa watani zao kwa miaka minne katika suala la ubingwa wa Bara sasa kimebaki kitu kimoja kinachowanyong’onyesha Yanga mbele ya Simba. Bado Yanga hawajui wajitetee vipi linapokuja suala la mashindano ya kimataifa. Miaka minne ambayo wameteseka kujitafuta majirani zao walitumia muda huo vizuri kutengeneza pengo kubwa kati yao katika mashindano ya kimataifa.

Kwa sasa jina la Simba sio geni kwa Waarabu au kule Afrika Kusini. Jina la Simba halishtui sana kuonekana katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho barani humu. Inawezekana wanaingia na kutoka, lakini kwa sasa wamejiweka katika daraja tofauti na Yanga linapokuja suala la mashindano ya kimataifa. Ni huku ambako Yanga wanapaswa kufikiria kufika kwa sasa. Kufika huku ambapo Simba wamefika kimataifa.

Kwa sasa vichwani mwao wanapaswa kuwaza jinsi watakavyokabiliana na mechi za Ligi ya Mabingwa. Kwanza kuweka malengo ya wapi wanataka kufika na mipango ya jinsi ya kufikia malengo waliyoyaweka. Nafikiri kwa kuanzia wahakikishe kwanza wanafika makundi kisha kutoka hapo waangalie wanafanya nini kuvuka makundi.


Ni ukichaa kuanza kufikiria kutwaa taji la klabu bingwa Afrika kwa sasa ukiwa hujafika hata makundi kwa zaidi ya miaka 20. Yanga wahakikishe wanafika makundi, kisha warejee tena makundi mwaka mwingine na mwaka mwingine tena. Baada ya hapo waanze kuzifikiria hatua za mtoano.

Lakini huko makundi wanafikaje? Ni swali linalopaswa kujibiwa sasa wakati huu msimu unaelekea kuisha. Huu ndio muda wa kufahamu wanarekebisha maeneo yapi katika kikosi na akina nani watawasajili.

Tatizo unaweza kuwauliza Yanga sasa hivi wanategemea kumsajili nani msimu ujao wakakuambia bado tunasubiri ripoti ya benchi la ufundi. Unakaa chini unafikiria, unasubiri ripoti ya benchi la ufundi sasa hivi kisha uanze kutafuta wachezaji lini? Muda wa kumfuatilia mchezaji unaupata wapi kama bado haujui utamsajili nani mpaka sasa?

Kufika muda huu Yanga walipaswa kufahamu wanamsajili nani na nani kuimarisha kikosi kuelekea mashindano ya Afrika msimu ujao. Kama bado, wanapaswa kukaa chini na benchi la ufundi muda huu na kuanza harakati za usajili.


 
Faida yao ni kwamba hawahitaji marekebisho makubwa sana katika kikosi chao. Nafikiri sehemu pekee ambayo Yanga hawapo vizuri ni katika benchi lao. Bado hawana mabadiliko ya kutisha sana wanapoamua kukiweka kikosi chao bora ndani ya uwanja. Lakini pia kitu kingine ni tofauti iliyopo kati ya upande wao wa ulinzi wa kulia na kushoto. Ipo tofauti kubwa sana kati ya upande wa kulia anaocheza Djuma Shaban na ule wa kushoto wanaocheza kina Shomari Kibwana na wenzake.

Bado nafikiri Shomari Kibwana hana ukomavu wa kutosha kukabiliana na winga hatari Afrika. Lakini hapohapo unatazama na uzoefu wa mabeki wa Yanga, kama Yanick Bangala anacheza katika eneo la kiungo Yanga wanabaki na beki mmoja pekee mwenye uzoefu na mashindano ya Afrika, Djuma Shaban pekee. Wengine hawana uzoefu wa kutosha. Mwamnyeto na Job bado hawajapata mechi za kutosha za kimataifa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad