Unaambiwa Watu 532,347 Waomba Ajira Kwenye Sensa



WATANZANIA 532,347 wametuma maombi Ofi si ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuomba kazi za muda za sensa ya watu na makazi tangu ajira hizo zilipotangazwa na serikali Mei 5, mwaka huu.

Akitoa taarifa za mwenendo wa maombi ya kazi hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Minja alisema tangu Mei 9, mwaka huu walipotangaza mara ya kwanza mwenendo wa uombaji wa kazi za muda hadi sasa unaendelea vizuri.

"Mwenendo wa uombaji wa kazi za muda za sensa ya watu na makazi mwaka 2022 unaendelea kwa kasi kubwa ikilinganishwa na wiki ya kwanza ya tangazo lilipotolewa," alisema.

Kati ya waombaji hao 532,347 ambao maombi yao yalipokelewa, waombaji 193,548 sawa na asilimia 36 ni waajiriwa katika sekta ya umma na binafsi. Huku waombaji 58,566 sawa na asilimia 11 wamejiajiri wenyewe na waombaji 280,233 sawa na asilimia 53 ni wale ambao hawana ajira.

Minja alisema mafanikio ya kuwa na waombaji wengi yamepatikana baada ya changamoto zilizotolewa na watumaji kufanyiwa kazi na serikali kwa wakati.

“Hadi jana (juzi) saa 7:00 mchana, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imepokea maombi hayo 532,347 kwa ajili ya nafasi 205,000 zilizotangazwa na serikali,” alisema.

Mei 9 mwaka huu NBS ilitoa tangazo la kwanza ambapo watu 119,468 walikuwa wametuma maombi ambapo ni sawa la ongezeko la maombi 412,879 hadi juzi. Minja alitoa mwito kwa wanaotuma maombi ya ukarani au usimamizi wa maudhui au usimamizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kufuata kikamilifu maelekezo yaliyowekwa kwenye tangazo la kazi.

Aidha, alisema waombaji wanatakiwa kuhakikisha wanajaza namba za simu na baruapepe ambazo wanazitumia hivi sasa ili waweze kupokea taarifa za akaunti zao za kuingia kwenye mfumo ili kukamilisha kutuma maombi.

Minja alisisitiza kwamba fomu ya maombi ya kazi za muda za sensa zinapatikana bila malipo na zinajazwa kupitia mfumo wa maombi ya kazi za sensa bila malipo.

"Waombaji wote wanakumbushwa kwamba maombi yote ya kazi yatumwe kabla ya Mei 19, 2022 saa 6:00 kamili usiku," alisema.

Naye Mratibu wa Sensa Taifa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu (NBS), Seif Kuchengo alisema kuna changamoto ndogo za mtandao kutokana na kutumika na watu wengi kwani mtu mmoja anahudumiwa takribani dakika 10.

Kuchengo aliwashauri watumaji maombi kutokata tamaa hata kama wengi wao hawana uzoefu wa kutuma maombi mtandaoni.

Mchakato wa kutafuta makarani ni sehemu muhimu ya maandalizi kufikia sensa ya watu na makazi itakayofanyika usiku wa kuamkia Agosti 23, 2022.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad