Na John Walter-Babati.
Viongozi mbalimbali wa Kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wengine zaidi ya 18 wa wilaya ya Babati mkoani Manyara wamekamatwa na polisi Jumatano Mei 25,2022 na kupelekwa katika kituo cha Babati kwa mahojiano.
Mwenyekiti wa CHADEMA mjini Babati Edgar Mwageni, amethibitisha kukamatwa kwa viongozi hao, akisema kuwa waliokamatwa ni pamoja na Mwenyekiti wa baraza la Vijana Taifa John Pambalu.
Bw Mwageni amesema viongozi hao walikamatwa wakiwa wanazunguka kuzungumza na baadhi ya wanachama wao mjini Babati wakihamasisha juu ya kampeni yao ya Kitaifa ijulikanayo kama "Join the Chain".
Amesema siku ya Jumanne waliketi kikao cha ndani katika Ukumbi wa AVIT mtaa wa mji mpya na kuzungumza juu ya umuhimu wa Katiba mpya bila usumbufu wowote.
Haijulikani ni sababu ipi ilisababisha maaafisa hao kukamatwa Lakini kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo anasema huenda walikamatwa kwa sababu ya mkusanyiko usiokuwa na kibali.
Kwenye Ukurasa wake wa Twitter Mratibu wa Uhamasishaji Baraza la vijana wa chadema Taifa (BAVICHA) Twaha Mwaipaya , ameandika "Tumekamatwa na polisi,tupo ofisi ya RPC mkoa wa Manyara,kosa ni kudai katiba mpya".
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Manyara Benjamin Kuzaga amesema ni mapema kuzungumzia tukio hilo.