VITA ya kuwania kiatu cha dhahabu sasa ipo kwa George Mpole wa Geita Gold na Fiston Mayele wa Yanga ambao wanafukuzana katika upachikaji wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara.
Hadi sasa Mpole ana mabao 11 akiwa nyuma bao moja kwa Mayele mwenye mabao 12 lakini kocha wa Geita, Fred Felix Minziro ameibuka na kusema kuwa straika wake ana nafasi kubwa ya kuwa Mfungaji Bora msimu huu huku wakiwa wamecheza mechi 21 kila mmoja.
Kocha huyo alisema hakuna ugumu kwa Mpole kufikisha idadi kubwa ya mabao msimu huu kutokana na maarifa na jitihada anazozionyesha.
“Muda wote akiwa uwanjani anafikiria kufunga kama alivyo Mayele na kimsingi ndicho kinachohitajika kufanyika kwa washambuliaji kwani sifa kuu ya mshambuliaji ni kufunga mabao.
“Ni ngumu kuwatofautisha washambuliaji hawa kwa muda huu kwani ukiangalia wapo kuwa uwanjani basi muda wowote unaweza kuona wakifunga na ndio maana namuona Mpole akifanya makubwa msimu huu” alisema Minziro
Naye Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema kuwa wote wana nafasi ya kutwaa kiatu lakini atakayekuwa na muendelezo mzuri wa kufunga basi ndiye atakuwa kinara.
“Kumaliza msimu ukiwa mfungaji bora inahitaji uwezo wa kufunga mabao angalau kila mechi au kila baada ya mechi moja basi ufunge mabao mawili zaidi lasivyo basi itakuwa ngumu na ndio maana wengine wataishia njiani kwenye vita hii ya mfungaji bora” alisema Mayay.
Ukiachana na Mayele na Mpole wengine wanaofuatia kwenye msimamo wa wafungaji bora ni Realints Rusajo wa Nmaungo (10), Meddie Kagere wa Simba (7) huku Vitalis Mayanga (Polisi Tanzania) na Saido Ntibazonkiza (Yanga) wakiwa na mabao sita kila mmoja.