Wabunge wapishana adhabu ya wanaume kuhasiwa wakibaka


By Habel Chidawali
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu amependekeza adhabu ya wabakaji na walawiti iwe ni kuhasiwa kwani adhabu ya miaka 30 ambayo hutolewa kwenye makosa hayo bado ni ndogo na haiwezi kumaliza matatizo.

 Mgalu amesema ulawiti na ubakaji vimekuwa janga kubwa na kuomba viongozi wa dini kusimamia maadili na kulibeba kwa uzito jambo hilo ambalo linaripotiwa kila wakati kwenye maisha ya kawaida.

Hii si mara ya kwanza kwa wabunge kuja na pendekezo la kutaka wanaume wahasiwe kwa madai kuwa itakuwa ni adhabu kubwa itakayowatisha na kuwapa uoga wanaume wenye tabia hiyo na wataacha.

Hata hivyo katika mchango wake Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu amepinga adhabu hiyo akisema itakuwa ni ukatili na mwisho wa siku itafanya Tanzania ikose mbegu njema na kwamba watoto wa kiume wanaonekana kutengwa wakati wao ndiyo wenye mbegu za kuzalisha.


 
Katika mchango wake kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu, mbunge huyo amesema kwa sasa nchi haiandaa kizazi chema badala yake kinaandaliwa kizazi chenye hofu kubwa.

“Jukumu la kulea watoto ni la wazazi lakini sisi wazazi ndiyo tunaacha kulisimamia jukumu hilo, viongozi wa dini mtusaidie kusimamia kwenye eneo ili wazazi tumrudie Mungu wetu kuokoa kizazi chetu,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake Msambatavangu amesema wazazi wamekuwa chanzo cha kuwatenga na kuwaacha watoto wa kiume kama mtu asiyekuwa na mchungaji kwani wanajengewa nyumba kwenye mabanda ya nyuma wakati watoto wa kike wanawekwa karibu na vyumba vya wazazi.


“Ukimweka mtoto wa kike jirani na chumba cha mzazi unataka kujua karudi muda gani, kafanya nini wakati yule wa kiume ambaye ndiyo aliyebeba mbegu za uumbaji unamweka banda la uani, karudi muda gani na anafanya nini hatujui na mwisho kinakuwa chanzo cha mgogoro,” amesema Msambatavangu.

Ametoa sababu za kupinga wabakaji wasihasiwe akisema utafika wakati watu watahitaji kuhemea mbegu kutoka nje lakini akazungumzia kuwa hata watoto wa kiume wanalawitiwa hivyo kuwepo na jukumu la kuwalinda huku akitoa sababu za upendeleo kwa watoto wa kike ikiwemo kujengewa shule kuliko wanaume ziachwe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad