Wadau Wausafiri Wapinga Ongezeko la Nauli Mabasi ya Mwendo kasi



WADAU wa Usafiri wa umma wamepinga pendekezo la ongezeko la nauli kwa watumiaji wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka wakisema ongezeko hilo linaenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa huduma hiyo ambayo ililenga kuwasaidia wananchi.

Pendekezo la kupandisha nauli liliwasilishwa jana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) maarufu mwendo kasi, Dk Philemon Mzee wakati akiwasilisha mada katika Mkutano wa Wadau kutoa maoni ya nauli za mabasi yaendayo haraka ili kuendana na gharama za uendeshaji kwa sasa.

Alisema kutokana na gharama za uendeshaji, malipo kwa wafanyakazi pamoja na ongezeko la hivi karibuni la kupanda kwa mafuta kutoka Sh 1,620 tangu mwaka 2016 hadi kufika Sh 3,258 mwaka 2022, wakala huo umeona ni muhimu kuongeza nauli ili kuendana na gharama hizo.

Aliongeza kuwa kupanda kwa gharama huko kumesababisha wakala kupendekeza nauli kupanda kutoka Sh 650 hadi 1,200 kwa Njia Kuu, kutoka Sh 800 hadi 1,500 kwa Njia Jumuishi, kutoka Sh 400 hadi 600 kwa Njia Mlishi na wanafunzi kutoka Sh 200 hadi 300.


“Upandaji huo wa nauli utakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma zetu ikiwemo kuongeza idadi ya mabasi mapya na yenye viyoyozi, kuongeza idadi ya mabasi yanayotumika kutoka katika idadi ya mabasi yaliyopo pamoja na kutengeneza mfumo utakaomwezesha abiria kujua liliko basi alitakalo kupitia simu yake ya mkononi,” alisema Dk Mzee.

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) kama mdau katika wasilisho lao lililowasilishwa na Leo Ngowi lilisema viwango vilivyopendekezwa na DART ni vikubwa na vinaweza kuleta maumivu kwa wananchi na kwamba vinakwenda kinyume na malengo ya uanzishwaji wake.

Alisema ni vizuri kupendekeza viwango vya nauli vitakavyoakisi gharama za uendeshaji pamoja na hali halisi ya maisha ya Watanzania kwani kinyume na hivyo itakuwa kuwakomoa wananchi ambao mwisho wa siku ndio watakaoumia.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam, Kismat Dhalla alisema hakuna haja ya DART kupandisha nauli kwa kuwa hata nauli zinazotozwa kwa sasa ni kubwa ikilinganishwa na uendeshaji wa chombo hicho.

Alisema mabasi yaendayo haraka hapa Dar es Salaam yana njia yake maalumu ambayo inayawezesha kutosumbuliwa na askari hivyo hawana gharama za uvunjaji wa sheria kama ilivyo kwa daladala na pia wanakwenda kwa haraka kutokana na kutosumbuliwa na foleni hivyo hakuna haja ya kuongeza nauli.

“Hizi gari zina uwezo wa kubeba abiria 80 kwa maana 40 waliokaa na 40 waliosimama lakini kwa utaratibu wa magari haya leo yanabeba abiria 200 mpaka 250, hapo unataka kuongeza nauli ya nini?”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad