Na Baraka Messa, Songwe.
WAHUDUMU wa afya wanafunzi katika hospital ya mji Tunduma wilaya ya Momba mkoa wa Songwe wamesababisha kifo cha mtoto wakati wa kujifungua.
Hayo yamebainishwa mei , 5 na mama mzazi wa mtoto ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetin katika hospital hiyo ya mji Tunduma baada ya kufanya mahojiano na Muungwana blog.
Alisema alifika hospitalini hapo mei tatu saa tatu usiku akiwa anaumwa uchungu, lakini alipofika Daktar alimwachia wauguzi wanafunzi ambao hawakutoa huduma nzuri kwake licha ya kuwaita mara kwa mara baada ya mtoto kuanza kutoka.
"Nilikuwa pekee yangu wakati mtoto anaanza kutoka nilipopiga kelele na kuomba msaada kwao walinambia niache kelele muda bado wa mtoto kuanza kutoka huku wakiendelea na shughuli zao bila kusogea kuja kunisaidia, baada ya kupiga sana kelele walikuja nikafanikiwa kujifungua lakini mtoto hakulia" alisema mama huyo.
Alisema wauguzi hao walimpeleka mtoto chumba cha oksjeni muda wa saa tisa usiku lakin , lakini akakabidhiwa mtoto saa moja asubuhi akiwa analia bila kupumnzika.
"Lakini cha kushangaza tulipofika nyumbani na mtoto wakati huo akiwa anaendelea kulia, mama wakati anamuogesha alimkuta na jeraha kichwani na uvimbe mkubwa , ndipo mama yangu mzazi akaamulu turudi hospitalini ambapo tulipewa dawa lakini kwa bahati mbaya mtoto wangu alifariki" alieleza mama huyo kwa uchungu.
Kwa upande wake bibi wa mtoto aliyefariki ambaye ni mama mzazi wa mama aliyefiwa na mtoto Ness Mwazembe alisema wakati akimuogesha mjukuu wake ndipo aligundua kuwa sababu za kulia sana mtoto zilisababishwa na maumivu aliyokuwa anayapata kutokana na jeraha la kichwani.
"Mwanangu alijifungua salama tukawa tunajiulza sasa hilo jeraha limetokana na nini? Lakini tulipofika hospital na mtoto ili kuhoji jeraha la mtoto limetokana na nini wale wauguzi walianza kuomba msamaha kuwa niwasamehe ,bila ya kunambia sababu" alisema Ness
Alisema ndipo alipoambiwa na baadhi ya ya watu hospitalini hapo kuwa waliokuwa wanamzalisha mtoto huyo ni wauguzi wanafunzi inasemekata walimdondosha wakiwa naye chumba cha oksijeni.
Mkuu wa mkoa wa Songwe Omary Mgumba alisema amepata taarifa za tuhuma hizo, ambapo tayari amemwagiza Mkuu wa wilaya hiyo ya Momba kuunda timu maalum kuchunguza tuhuma hizo .
"Hili sio tukio la kwanza wala la pili katika Hospital ya mji Tunduma , serikali hatupuuzi malalamiko ya wananchi ambao ndio tunawaongoza , baada ya uchunguzi utakaofanyika tutatoa majibu ya kifo cha mtoto huyo ili wahusika ikiwa walifanya ni uzembe wachukuliwe sheria" alisema mkuu wa Mkoa.
Aidha Mgumba amewataka watumishi wa Serikali hasa wahudumu wa afya kutoa huduma nzuri na lugha nzuri pindi wanapotoa huduma za kitabibu kwa wananchi.