Wanaume wawili na mwanamke mmoja walipatikana wamekufa huku wakiwa wameshikana mikono katika nyumba ya wageni iliyoeneo la Pipeline Nairobi.
Mmoja wa wanaume walioaga alikuwa anavuja damu mdomoni na puani wakati miili yao ilipogunduliwa Jumatatu alasiri.
Polisi walisema tukio hilo ni kitendawili lakini wakaongeza kuwa wanachunguza vifo hivyo ili kubaini kilichotokea pale.
Maafisa wa upelelezi wanaoshughulikia tukio hilo walisema wanashuku kuwa huenda itikadi kali zilisababisha tukio hilo.
Hata hivyo, hakukuwa na dalili ya mapambano au kuvunjwa kwa chumba hicho, jambo ambalo lilifanya polisi kuhitimisha kwa sasa kuwa huenda walijitoa uhai.
Waathiriwa walitambuliwa kama Philip Murefu Simiyu mwenye umri wa miaka 63, Boniface Muchiri Waruiru mwenye umri wa miaka 28 huku mwanamke akiwa bado hajatambuliwa.
Mmiliki wa chumba cha wageni cha Chairman Lounge alisema watatu hao waliingia mwendo wa saa sita usiku wa kuamkia Jumatatu .
Walilipia chumba kile, wasimamizi walifikiri kuwa watatu hao walitaka kujiburudisha.
Watatu hao hata hivyo walikosa kutoka nje ya chumba kile Jumatatu alasiri kama ilivyotarajiwa.
Mhudumu aliyekwenda kuwaangalia alisema hawakujibu na akalazimika kupiga simu kwa polisi ambao waliingia kupitia dirisha mwendo waa saa nane alasiri .Hapo ndipo miili hiyo ilipogunduliwa.
Kilichopelekea tukio hilo bado hakijajulika. Miili hiyo ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo uchunguzi wa maiti utafanyika.
Maafisa wa upelelezi wa mauaji walisema wamekuwa wakifuatilia familia za marehemu ili kuelewa ni nini huenda kilitokea.
"Uchunguzi wa maiti utabaini ikiwa walikunywa sumu au ni nini hasa kilichotokea chumbani. Kwa sasa, hatujui ni nini kilisababisha kisa hicho,” alisema mkuu wa DCI wa Nairobi Paul Wachira.
Aliongeza uchunguzi wa maiti pia itawasaidia kumtambua mwanamke huyo.