Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima
Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likiwakamata watu 31 kwa tuhuma za kujihusisha na na vitendo vya kihalifu maarufu ‘Panya Road’, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewaonya wazazi wanaozembea kwenye malezi na hivyo kuzalisha watoto wahalifu.
Alieleza hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Mbezi Luisi kuelekea Siku ya Familia inayoadhimishwa ifikapo Mei 15 ya kila mwaka.
Alisema wakati Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji watu hao, wizara yake itafanya uchunguzi wake ili kubaini kama kuna wazazi wanahusika kwa namna moja au nyingine na matukio yanayofanywa na watoto wao.
“Hili ni tatizo linalotokana na wazazi, mtoto haonekani na mzazi hahangaiki kumtafuta. Upo uwezekano wa baadhi ya watoto kutumwa na wazazi au kufundishwa,” alisema Dk Gwajima.
Juzi wakati akizungumza na wanahabari, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema watu hao 31 walikamatwa katika operesheni maalumu ya msako wa mtaa kwa mtaa, dhidi ya vijana wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu.
Alisema operesheni hiyo ambayo ni endelevu ilianza Aprili 27, 2022 na imefanikiwa kuwakamata wahalifu hao, wengi wakiwa ni vijana kati ya miaka 13 hadi 20, ambao hutumia mapanga, visu, nondo na mikasi mikubwa wanapofanya uhalifu.