Wazururaji wasakwa stendi ya Magufuli



Dar es Salaam. Katika kuimarisha usalama wa abiria na mizigo yao kwenye Kituo cha Mabasi cha Magufuli, uongozi wa kituo hicho umeanza operesheni maalumu ya kuwakamata wapigadebe, wazururaji na wakatisha tiketi wanaofanya shughuli hizo nje ya kituo.

Operesheni hiyo iliyoanza kwa takriban mwezi mmoja sasa inafanyika mchana na usiku baada ya uongozi kupokea malalamiko kutoka kwa abiria ya kuibiwa mizigo na kulanguliwa bei ya tiketi.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja msaidizi wa kituo hicho, Laurent Cheche alisema suala la kuongezeka kwa ulanguzi kunachagizwa na ushindani wa kibiashara uliopo ambapo kuna baadhi ya watoa huduma hutoka na vitabu kwenda kukatisha tiketi nje ya kituo.

“Tumeanzisha msako huu kwa lengo la kuwaondoa wapigadebe, kwani shughuli hizo haziruhusiwi kufanyika kwa mtindo huo na pia wanaisababishia Serikali kukosa mapato,” alisema Cheche.


 
Alisema kuna magari ambayo abiria hawayataki kwa sababu ya ubora na uhakika wake wa kuwafikisha mwisho wa safari, kwa hiyo wapigadebe hao wamekuwa wakitumika kuwarubuni na kuwalaghai watu wakapande kwenye magari hayo.

Alisema ili kuhakikisha wanafanikiwa kuwazuia, wameanzisha vituo vinne vya kuwakamata, ikiwemo magari yanayoenda mikoa ya Kaskazini, mlango wa kuingilia magari madogo na mbele ya kituo hicho ambapo askari wanazunguka kuimarisha ulinzi muda wote.

“Tayari watu 25 wamekamatwa na wamechukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwamo kupigwa faini na wengine wanafunguliwa mashtaka kwenye mahakama ya jiji iliyopo Posta,” alisema Cheche.


Taboa waunga mkono

Mkurugenzi wa Habari Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo alipongeza kufanyika kwa msako na kueleza kuwa kuna baadhi ya watu wananunua mavazi na kuweka nembo ya kampuni ya mtu ili apate abiria. Alisema hali hiyo inaleta usumbufu kwa abiria kwa sababu wanashindwa kuelewa mtu sahihi wa kuwahudumia.

“Akishawapata anawakatia tiketi zisizokuwa halali, akifika nao ndani ya kituo kwa sababu biashara ngumu, wale abiria wanauzwa kwa basi jingine huku muuzaji (mpiga debe) akijipatia fedha ya ziada kwa sababu kaleta abiria wengi kwa wakati mmoja.

“Mara nyingi abiria wa staili hii wanajikuta wakipanda mabasi ambayo siyo chaguo lao, ila kwasababu wanakuwa wamekwishatoa fedha zao wanakosa nguvu ya kukataa,” alisema.

Polisi Kinondoni

Kamanda wa Mkoa wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhan Kingai alisema wamewasambaza askari wa kutosha kufanya doria ya kuwakamata wote wanaofanya kazi hizo nje ya kituo hicho.


 
“Rai yangu mtu kama huna kazi usiendelee kupiga debe, tafuta shughuli nyingine za kufanya kwani wamekuwa wakifanya kazi hizo na kupora mabegi ya abiria na kutokomea kwenda kusikojulikana,” alisema Kingai.

Alisema katika msako huo wanakamatwa wengi na kupelekwa mahakama ya jiji na kwamba askari wa mkoa huo wako makini kulinda usalama wa raia kuhakikisha hawabughudhiwi.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaoendesha shughuli hizo nje ya stendi ambao hawakutaka majina yao kutajwa walidai kufukuzwa si jambo sahihi kwa kuwa wanaoendeleza vitendo hivyo si wote na Serikali ina uwezo wa kuwadhibiti.

“Sisi wengine hatuna kazi, tunategemea kupitia kazi hii kupata riziki, sasa unapotufukuza tutaishije na tuna familia. Walipaswa watumie busara tushirikiane kwa sababu wanaowaibia abiria na kuwapandishia nauli tunawajua,” alisema.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad