WINGA machachari wa RS Berkane ya nchini Morocco, Tuisila Kisinda ameonekana kuwagawa mabosi wa timu hiyo, katika mipango ya kutaka kumrejesha kikosini hapo msimu ujao.
Hivi karibuni tetesi zilienea za winga huyo kurejeshwa Yanga katika msimu ujao kwa kile kilichoelezwa kuachana na klabu yake ya Berkane.
Yanga ilimuuza Kisinda msimu uliopita kwenda Berkane kwa dau la Sh mil 250 sambamba na kuigharamia timu hiyo kambi nchini Morocco ambao walikaa kwa wiki moja na nusu.
Chanzo cha habari, kutoka ndani ya Kamati ya Mashindano na Usajili ya timu hiyo, kimeliambia Championi Jumatano kuwa, bosi mkubwa Yanga ameshauri kuachana na Kisinda na badala yake kumtafuta winga mwingine tishio.
Chanzo hicho kilisema kuwa bosi huyo anaamini wapo mawinga wengine wengi Ukanda wa Afrika Magharibi kutoka nchi za Ivory Coast, Nigeria na Ghana wenye viwango zaidi ya Kisinda.
Kiliongeza kuwa bosi huyo ameahidi kutafuta winga mwenye ubora mkubwa zaidi ya Kisinda atakayefanya makubwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki msimu ujao.
“Yupo bosi mkubwa mwenye ushawishi wa usajili ndani ya Yanga ambaye yeye ameshauri kuachana na Kisinda na badala yake kumleta mwingine mwenye kiwango bora zaidi yake.
“Anakiri kukubali kiwango cha Kisinda, lakini kwa malengo ambayo tuliyokuwa nayo Yanga hivi sasa katika michuano ya kimataifa tutakayoshiriki msimu ujao ya kufika nusu fainali, basi winga huyo hahitajiki.
“Hivyo basi kama uongozi, hilo suala lipo kwa uongozi ambao wameshindwa kulifikia muafaka hadi hapo baadae lakini uwezekano wa kurejea tena Kisinda ni mdogo Yanga,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo, alisema kuwa: “Kisinda bado mchezaji halali wa Berkane mwenye mkataba, hivyo sitakuwa katika nafasi nzuri kuzungumzia hilo.”
Na Wilbert Moland