KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, amesema wameenda kupambana kutafuta pointi muhimu dhidi ya Ruvu Shooting katikka mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga imewasili Kigoma tayari kuvaana dhidi ya wenyeji wao, Ruvu Shooting kwenye mchezo wa ligi hiyo utakaopigwa kesho, Jumatano katika dimba la Lake Tanganyika, mkoani humo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaze alisema baada ya Kariakoo 'Derby', walirejea mazoezi kufanyia kazi mapungufu yao ikiwamo kuongeza umakini kwa safu ya ushambuliaji katika umaliziaji wa nafasi wanazotengeneza.
Alisema wanahitaji kupambana kila mechi kutafuta pointi tatu ili kufikia malengo yao ya Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu msimu huu, lakini kuweka rekodi ya kutopoteza mechi.
“Siwezi kusema kwamba hatutapoteza ila mipango yetu ni kuona tunapambana na ikiwezekana tunaweka rekodi ya kumaliza ligi bila ya kupoteza kwa sababu ligi imekuwa ngumu, kikubwa tujitume ili kutafuta matokeo mazuri katika michezo iliyopo mbele yetu,” alisema Kaze.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema wanakwenda kuvunja mwiko wa Yanga.
"Hatuwezi kuwapelekea mechi mashabiki wa Kigoma, halafu tufungwe kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, naona Simba wameshindwa kuwafunga Yanga, sisi tunakwenda kutekeleza hilo kwa vitendo, hakuna mbwembwe nyingi, tutavunja mwiko wa kutofungwa na wale wanaotetema, wanatetemeka kwa mashaka," alisema Masau.