Yanga Unaambiwa Waanza Kuitolea Macho Michuano ya CAF, Mkakati Kabambe wa Kuongeza Wachezaji Wahitajika



KIKOSI cha Yanga kinapambana kujimilikisha taji la Ligi Kuu msimu huu, huku ikiwa tayari na tiketi ya michuano ya CAF msimu ujao na kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ameanza kupendekeza mastaa anaowataka ili kumbeba kimataifa.

Lakini, wakati Nabi akianza kupiga hesabu zake kijanja, nyota wa zamani wa timu hiyo wamekiangalia kikosi na kutoa msimamo juu ya wachezaji wapya wanaohitajika kuifanya iwe tishio zaidi ya ilivyo msimu huu.

Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 56 baada ya mechi 22 keshokutwa, itakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons.

Tangu ilipofungwa na Azam katika Ligi Kuu Aprili 25, mwaka jana, imecheza mechi 29 bila kupoteza, ikiifukuzia rekodi ya msimu uliopita ilipocheza mechi 32 bila kupoteza na pia kuitafuta rekodi ya Azam ya kucheza mechi 38 kati ya 2012-2014. Kutokana na kuwa na uhakika wa michuano ya CAF, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’, alisema Yanga inahitaji kuongezwa nguvu ili kufanya vizuri zaidi na kufika mbali zaidi ya ilipokwamia msimu huu ilipotolewa raundi ya awali na River United.


“Yanga inatakiwa kusajili washambuliaji wapya wawili wenye uhakika wa kufunga zaidi ya Fiston Mayele, beki mmoja wa kushoto na wa kati wenye uzoefu mkubwa sio kutoka ligi ya ndani wote uwezo wao ni sawa,” alisema.

“Kwa sasa yupo Mayele ambaye tayari mabeki wa timu pinzani ni kama wamemuundia tume wakimkaba vilivyo na asipofunga timu inayumba, nadhani kocha hilo ameliona anahitaji kulifanyia kazi mapema.”

Makumbi alisema beki wa kati lazima awe mrefu na mwenye nguvu ili amuongezee nguvu Bakari Mwamnyeto na kwa mabeki wa pembeni kushoto kuna tatizo, japo hata kulia kuna Djuma Shaban na Kibwana Shomary.

Naye winga wa kimataifa aliyekipiga Yanga na Simba, Akida Makunda, alisema Yanga inatakiwa kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji na kiungo mshambuliaji. “Viungo waliopo ni wazuri lakini akikosekana mmoja unaona timu inabadilika uchezaji hivyo wanatakiwa kuongeza nguvu eneo hilo,” alisema.

MSIKIE NABI

Kocha Nabi alisema anatambua kazi aliyonayo msimu ujao kimataifa, lakini kwa sasa akili yake ni kumalizia mechi ili kubeba ubingwa, na suala la usajili ni mapema mno kusema atawaacha nani na kusajili kina nani, japo ameshatoa maelekezo kwa uongozi.

“Ukifika wakati wa usajili sitasema majina nahitaji mchezaji gani, bali nitatoa sifa za nyota mpya ninayemhitaji kulingana na eneo tunalotaka kuongeza nguvu na hilo ndio lilisaidia kupata waliokuwa bora kama msimu huu,” alisema. Baadhi ya wachezaji walio katika nafasi kubwa ya kupigwa chini kwa viwango vyao na ishu za mikataba ni Chico Ushindi, Deus Kaseke, David Brayson, Heriter Makambo na kipa Erick Johola.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad