Zitto Kabwe Amwaomba Rais Samia Kukutana na Wamachinga



Mwanza. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na wamachinga ili kuwasikiliza na kujua changamoto zinazowakabili, badala ya kusikiliza ushauri wa wasaidizi wake ambao baadhi wamekiuka maelekezo yake kuhusu kundi hilo.

Akizungumza wakati wa kongamano maalumu la operesheni “Tume huru kuelekea Katiba Mpya” iliyofanyika jijini hapa jana, Zitto alisema baadhi ya wasaidizi wa Rais ngazi ya halmashauri, wilaya na mikoa wamekiuka agizo la mkuu huyo wa nchi la kuwapanga wamachinga kwa kuwapeleka katika maeneo yasiyofikika kirahisi.

Huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo lililohudhuriwa na washiriki kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Zitto alitoa mfano wa Jiji la Mwanza ambalo wafanyabiashara hao wamehamishiwa eneo la dampo la Buhongwa, karibu kilomita sita kutoka katikati ya jiji.

“Namuomba Rais Samia afanye ziara akianzia Mwanza ili azungumze na wamachinga na achukue maamuzi,” alisema Zitto.

Sera ya wamachinga

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo, alisema chama chake kinatarajia kutangaza na kuzindua sera ya wamachinga ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni itakayotoa mwongozo na mbinu za kushughulikia kero na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo .

“Chama cha ACT Wazalendo kitakuwa chama cha kwanza kuandaa sera na mwongozo wa kushughulikia masuala ya wamachinga, kwa sababu hadi sasa hakuna chama kikiwemo CCM yenyewe yenye sera na mwongozo huo,” alieleza Zitto aliyeambatana na viongozi wengine wa juu wa chama hicho waliopiga kambi jijini Mwanza katika kampeni ya kuimarisha chama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad