Mpole amemaliza na mabao 17 na assisti tatu katika michezo 30 ya Ligi Kuu ya NBC msimu huu.
Mwanza. MSHAMBULIAJI wa Geita Gold, George Mpole ameibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2021/2022 baada ya kufunga mabao 17 katika michezo 30.
Mpole amejihakikishia nafasi hiyo baada ya kutupia bao muhimu leo katika mchezo wa mwisho timu yake ikimaliza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga huku mpinzani wake wa karibu, Fiston Mayele wa Yanga aliyemaliza na mabao 16 akishindwa kucheka na nyavu leo wakati mabingwa hao wa Ligi wakiichapa Mtibwa Sugar 1-0.
Akizungumza baada ya mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Mpole amesema wakati msimu unaanza alijiwekea malengo ya kuwa mfungaji bora hivyo kutimia kwa jambo hilo ni mafanikio makubwa huku akishukuru Mungu kwa kumuepusha na majeraha.
"Najiskia vizuri ni kitu ambacho nilikiwekea malengo na ilikuwa ni ndoto yangu tangu naanza mechi yangu ya kwanza ya Ligi nilijiwekea kuwa mfungaji bora kwahiyo nashukuru Mwenyezi Mungu ameweza kuniepusha na majeraha mpaka nimemaliza nikiwa mfungaji bora". amesema Mpole na kuongeza,
"Ligi ya mwaka huu ilikuwa ni ngumu sana tofauti na misimu ya nyuma ushindani ulikuwa mkubwa tumeona hadi mechi za mwisho ndizo zimetoa maamuzi ya timu za kushuka daraja na nafasi nne za juu, nawapongeza TFF (shirikisho la soka Tanzania) waendelee kuboresha zaidi".
Akizungumzia uwezekano wa kusalia Geita Gold, Mpole amesema mashabiki wavute subira kwani muda ukifika watafahamu chama lake jipya huku akikiri kuwa kuna ofa tayari anazo mkononi na anazifanyia kazi.
"Muda ukifika kila mtu atajua timu gani nakwenda, muda bado upo kuna ofa ambazo tulikuwa tunazifanyia kazi zikikaa sawa watu watajua ni wapi naelekea". amesema Mpole.