Aliyevuliwa Umeya Moshi Autamani Tena..Raibu Achukua Fomu ya Umeya



Juma Raibu akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Meya Manispaa ya Moshi, Raibu aliondolewa kwenye nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura ya siri na madiwani. Picha na Florah Temba
Moshi. Meya wa zamani wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Juma Raibu aliyevuliwa wadhifa huo baada ya kupigiwa kura za siri na madiwani za kukataliwa amejitokeza tena kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Juma Raibu aling'olewa katika wadhifa huo Aprili 11 mwaka huu, baada ya madiwani kupiga kura za siri na kati ya kura 28 zilizopigwa, 18 zilikataa asiendelee na wadhifa huo huku 10 zikimtetea abaki katika nafasi hiyo aliyodumu nayo tangu ulipokamilika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Tuhuma zilizomng'oa Raibu ni madai ya kuhudhuria sherehe ya kijana mmoja anayedaiwa kushiriki mapenzi ya jinsia moja, kutumia vibaya ofisi yake, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuruhusu ujenzi holela na kutumia fedha nje ya utaratibu.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Moshi mjini, Raibu amesema ameamua kurudi kuwania nafasi hiyo kwa kuwa toka ameondolewa kwenye nafasi hiyo, baada ya kuona Moshi imepoa na kuwepo kwa vurugu nyingi.


"Moshi imelala, siyo Moshi niliyokuwa nikiiongoza, nimeona ni wakati wa kurudi kuchukua nafasi hii, ninaamini tutashirikiana na madiwani katika kuiendeleza Moshi.

Amesema zaidi ya wananchi 500 wamefika nyumbani kwake kumuomba na kumchangia ili aweze kurudi kugombea nafasi hiyo.

"Niliwakatalia wananchi na kutaka kupeleka fedha hizi kutoa sadala, lakini walikataa wakataka nije nichukue fomu na niwaambie nipitishwe au nisipitishwe, nitaendekea kuwa mwanachama wa CCM"


Katibu wa CCM Moshi Mjini, Ibrahim Mjanakheri amesema tangu kuanza mchakato wa kuchukua fomu Juni 12, tayari wamechukua madiwani nane.

Amewataja Madiwani hao kuwa ni Apaikunda Nabuli, Francis Shio, Zubery Kidumo, Charles Lyimo, Stuart Nkinda, charles Mmbando, Nasibu Mariki na Juma Raibu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad