Baada ya Nabi Kumpiga Chini Saido Sasa Anaefuata ni Huyu


NI rasmi kwamba Yanga imetangaza kuachana na Saido Ntibazonkiza. Siyo huyo tu imefuta pia mpango wa kumsajili beki wa Uganda, Mustafa Kizza sababu kubwa ikitajwa kwamba amekaa nje ya mechi za ushindani kwa muda mrefu.

Lakini Kocha Nabi ameliambia Mwanaspoti jana kwamba anataka beki mmoja matata sana mmwaga maji kule kushoto.

Nabi ambaye ana uraia pacha wa Ubelgiji na Tunisia, ameliambia Mwanaspoti kuwa kikosi chake kuelekea mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanahitaji kuwa imara zaidi ili kuepuka fedheha kama ya msimu uliopita.

Alisema anahitaji beki wa maana wa kushoto ambaye atakuwa na sifa za kujua kuzuia na kupiga krosi kali zenye madhara kwani kimataifa wanataka kuingia na miguu miwili msimu huu.

Alisema beki huyo akiwa wa kigeni atafurahia zaidi na ameshawapa viongozi wa usajili kazi na yeye pia yuko sokoni.

Akili hiyo ya Nabi inakuja ikiwa zimepita siku tatu tangu waing’oe Simba kwenye hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Azam Shirikisho na sasa wakiwa na nafasi kubwa ya kwenda kubeba Ligi Kuu Bara.

Yanga ikicheza mechi hiyo ya Simba ilizalisha krosi tatu pekee za upande wa kushoto ambao alicheza Kibwana Shomari ambaye hata hivyo aliumia dakika ya 60 ya mchezo huo kwa kugongana na Kibu Denis wa Simba.

Katika krosi hizo tatu Kibwana alipiga mbili huku moja akipiga Farid Mussa aliyeingia badala yake nafasi ambayo mshambuliaji Heritier Makambo licha ya kuruka akiwa mwenyewe alishindwa kufunga.


“Tunahitaji sana beki mzuri wa upande wa kushoto nawaamini viongozi wangu tunahitaji mtu wa kusaidiana na Kibwana,” alisema Nabi ambaye kwa sasa ni mwenye furaha kwani anakaribia kutimiza malengo yake ya kimkataba.

“Kibwana ni mtu bora sana ana matumizi mengi katika timu yetu lakini tunahitaji nguvu ya Farid pia kwa eneo la juu,kwahiyo beki anayekuja anatakiwa kuwa juu ya wote katika kujua kuzuia na kupandisha mashambulizi,”alisema Kocha huyo ambaye hivi karibuni Nabi aliliambia Mwanaspoti kwamba hatasajili mchezaji yoyote ambaye hajacheza mechi za ushindani muda mrefu hata awe na jina kubwa kiasi gani.

SAIDO APIGWA CHINI

Yanga jana ilitangaza kumuacha Saido ikiwa ni sikuchache baada ya kumuondoa kambini kwenye mechi dhidi ya Simba. Licha ya kwamba hawakufafanua chanzo lakini Mwanaspoti linajua alikuwa anashinikiza kupewa mkataba wa miaka miwili wakati klabu ikitaka kumuongezea mwaka mmoja tu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad