Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC Barbara Gonzalez leo Jumanne (Juni 14) ametembelea eneo la Uwanja wa Mo Simba Arena lililopo Bunju jijini Dar es salaam, akiongozana na msanifu majengo (architect).
Barbara alifanya ziara hiyo iliyohudhuriwa pia na Waandishi wa Habari kwa lengo la kukagua mipaka na eneo ambalo litatumika kwa ujenzi wa Uwanja Mo Simba Arena, ambao kwa sasa unatumika kwa mazoezi ya vikosi vya klabu hiyo.
Akiwa katika zoezi la ukaguzi wa maeneo ya Uwanja huo Barbara alisema, zoezi la kujenga majukwaa na miundo mbinu mingine ya Uwanja wa Mo Simba Arena wamelidhamria na zimebaki siku chache kabla ya Bodi ya Wakurugenzi itakayokutana Ijumaa (Juni 17) ili kumpitisha mkandarasi.
“Tuna mpango wa kuboresha uwanja wa Mo Simba Arena, kuweka uzio na majukwaa ili watu wakija hapa wafurahie zaidi “
“Kazi ya bajeti tutapata kwa Architect lakini naona ikiwa chini ya Bilioni 2 kwa uboreshaji wa viwanja hivi vya mazoezi”
“Mimi kama CEO kazi yangu ilikuwa ni kutengeneza michoro kazi iliyobaki ni kuwaachia bodi kutoa marekebisho au kutoa ruhusa kuendelea,”
“Baada ya ruhusa ya bodi sasa ndiyo mtaona mambo yakianza kwenda kwa kasi zaidi sasa,” alisema Barbara Gonzalez