MTU mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa akiwamo Mwanafunzi wa Shule ya Msingi baada ya basi la Kampuni ya Geita Express kuacha njia na kugonga nyumba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP. Lucas Mwakatundu, akizungumza na waandishi wa habari leo alisema ajali hiyo imetokea jana saa 2:20 usiku katika Kijiji cha Mkiwa wilayani Ikungi mkoani hapa Barabara Kuu ya Dodoma- Singida
ambapo imehusisha Basi lenye namba T 417. CTD aina ya Scania.
Alimtaja aliyefariki kuwa ni Alon Basili (36), mkazi wa Kijiji cha Mkiwa ambapo mwili wake umehifadhiwa katika Zahanati ya Ikungi.
Kamanda Mwakatundu amewataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Martha Jeremiah (36) mkazi wa Kijiji cha Mkiwa na Nassoro Abdallah (11) ambaye ni Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkiwa.
Aliongeza kuwa majeruhi wote walikuwa wamelala ndani ya nyumba hiyo na kwamba wamelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Gasper iliyopo Itigi Wilaya ya Manyoni.
Kamanda Mwakatundu alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa dereva wa basi hilo.
Alisema kufuatia ajali hiyo Jeshi la Polisi linamshikilia dereva wa basi hilo,Boniphace Machage kwa mahojiano ambayo yakikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kamanda Mwakatundu ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya usafiri kufuata sheria,kanuni na taratibu zilizowekwa kusimamia usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuepukika.