Bosi Simba Aanika Mkataba wa Chama, Kocha Hakumtaka Hakuwepo katika Mipango Yake




MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji ‘KD’ amesema kuwa kiungo mshambuliaji Mzambia, Clatous Chama hakuwepo katika mipango ya usajili wa dirisha dogo katika msimu huu.

 

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu kiungo huyo aondolewe kambini Mwanza na kurejea nyumbani kwao Zambia.

 

Kiungo huyo aliondolewa kambini ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo wa Kariakoo Dabi wa Nusu Fainali ya Kombe ya FA dhidi ya Yanga uliochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na Simba kufungwa bao 1-0.

 


Kiungo wa Simba, Mzambia Rally Bwalya (kulia) akiongea na Chama.

 

Akizungumza na moja ya redio kubwa hapa nchini, Dewji alisema kuwa mipango iliyokuwepo katika dirisha dogo ni kumsajili mshambuliaji wa kigeni pekee mwenye kiwango bora na uzoefu wa michuano ya kimataifa.

 

Dewji aliongeza kuwa walipanga kusajili mshambuliaji kutokana na mapendekezo ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco, maalum kwa ajili ya kumtumia katika Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Aliongeza kuwa Chama hakuwa sehemu ya kuhitajika katika usajili huo kutokana na kanuni kumbana za kucheza michezo ya kimataifa, kwani alicheza akiwa RS Berkane ya nchini Morocco.

 

“Malengo ya timu yalikuwa ni kumsajili mshambuliaji kwa ajili ya michuano ya kimataifa na sio kiungo ambaye ni Chama, tumetumia gharama kubwa kufanikisha usajili wake.

 

“Na kocha ndiye aliyependekeza usajili wa mshambuliaji na sio kiungo, lakini baadae tukashangaa kumuona akisajiliwa wakati hakuwepo katika uhitaji.

 

“Chama ni mchezaji mzuri lakini hakuwa katika mipango ya klabu, safu yetu ya ushambuliaji ndio ilikuwa ikihitaji maboresho kimataifa,” alisema Dewji.

Stori na Na Wilbert Molandi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad