Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson
CHAMA cha Chadema, kimemwandikia barua Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kumkumbusha kuhusu utekelezaji wa barua yake ya tarehe 12 Mei 2022, iliyoomba awaondoe bungeni wabunge viti maalum 19 ambao kimewavua uanachama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Ni baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, jana Jumatano, kuyaondoa maombi ya wabunge hao ya kufungua kesi kwa ajili ya kupinga kuvuliwa uanachama, ambapo Spika Tulia alisita kuwaondoa bungeni hadi maombi yao yatakapotolewa uamuzi.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi, tarehe 23 Juni 2022 na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, amesema Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amemwandikia barua kumtaarifu kwamba maombi hayo yameshatolewa maamuzi.
“Barua yetu ya tarehe 12 Mei 2022, iliyobeba maazimio ya Baraza Kuu juu ya rufaa zilizokuwa za wanachama 19 wa Chadema, tulimtaka Spika kutekeleza kifungu cha katiba cha kutambua kwamba, ili mtu awe na hadhi ya ubunge lazima awe ametokana na chama cha siasa na anapopoteza uanachama wake kimsingi anapoteza ubunge wake,” amesema Mwalimu.
Mwalimu amesema “kwa hiyo tulimtaka atekeleza hivyo akaeleza kuna jambo mahakamani na sisi tumemkumbusha lile jambo mahakaani limemalizika kwa utaratibu huu.”
Mwalimu amesema, nakala ya barua hiyo imetumwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Tumemwandikia barua jana jioni baada ya hukumu ile na tumeituma kwa barua pepe rasmi kumuelezea hukumu ile na kumtaka kuitekeleza barua ya Chadema ya tarehe 12 Mei 2022. Nakala imepelekwa kwa msajili wa vyama vya siasa na mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC. Tumeshatimiza wajibu,” amesema Mwalimu.
Wabunge waliofukuzwa Chadema, ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Halima Mdee, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya.
Aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega
Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.
Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Baada ya Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao za kupinga kuvuliwa uanachama, Mdee na wenzake walitinga mahakamani kufungua maombi ya kufungua kesi kwa ajili ya kupinga hatua hiyo, huku wakiiomba waweke zuio la wao kuondolewa bungeni hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Lakini jana Mahakama hiyo mbele ya Jaji John Mgetta, aliyatupa maombi hayo kwa sababu yalikiuka misingi ya kisheria kwa kukosea kuandika jina la mjibu maombi wa kwanza (Chadema).
Pius Mhehe
8min
Zuio lao limeisha Jana lakini spika anatakiwa awatoe bungeni Kama wanahitaji kwenda mbele kisheria wanatakiwa wawe nje kwa sababu hawana chama mpaka hapo watakapopewa Haki na mahakama nyingine watakayokatia rufaaZaidi