MKUTANO wa Kanda ya Victoria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliofanyika mkoani Geita, umemalizika kwa kuiomba serikali kuondoa zuio la kutofanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa ili kutoa fursa ya kujiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao.
Kanda hiyo ya CHADEMA inaundwa na mikoa mitatu ya Mwanza, Geita na Kagera.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, aliwasilisha hoja yao hiyo juzi wakati akifunga mkutano na kutoa majumuisho ya mkutano huo.
Mnyika alisema hali ya kisiasa kwa sasa ni nzuri lakini CHADEMA ingependa kuona zuio lililowekwa la kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa linaondolewa ili kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma na kuwajengea uwezo wananchi kupiga kura.
Alisema CHADEMA inaridhia kuendelea kwa mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama chao kwa lengo la kuleta maridhiano ya kisiasa nchini.
Alisisitiza kuwa suala la kupatikana kwa Katiba Mpya na Tume huru ya Uchaguzi ni ajenda endelevu kwa chama chao.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Pambalu, akimkaribisha Mnyika, katika mkutano huo, aliwashukuru wanachama wenzake na viongozi wa kada zote kwa kumuunga mkono katika operesheni yake ya kusaka Katiba Mpya, jukumu lililokuwa limekabidhiwa kwa BAVICHA na uongozi wa juu wa chama chao.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita, Fabian Mahenge, aliyekuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisema sasa kuna nuru iliyoanza kujitokeza ya matumaini ya hali ya kisiasa nchini, hasa kwa kambi ya upinzani na kuwa ni wakati mwafaka kwa upinzani kujijenga upya kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.