Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeweka pingamizi katika maombi ya Halima Mdee na wenzake ya amri ya muda ya Mahakama kuizuia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Spika wa Bunge kuwavua ubunge.
CHADEMA, imeweka pingamizi hilo Mahakama Kuu ambayo imetoa amri ya kuwa hadhi ya Wabunge hao itabaki kama ilivyo mpaka siku iliyopangwa ya usikilizwaji wa pingamizi hilo, Juni 29, 2022.
Halima Mdee na wenzake wamefungua maombi katika Mahakama Kuu dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema kuomba ridhaa ya kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wa CHADEMA.
Aidha, amoja na maombi hayo ya ridhaa namba 27 ya mwaka 2022, pia wamefungua maombi ya amri ya zuio dhidi ya NEC na Spika, kutochukua hatua dhidi ya uamuzi wa CHADEMA wa kuwavua uanachama ambayo yaliyopangwa kusikilizwa na Jaji Mustapha Ismail.
Hata hivyo, leo Jumatatu Juni 27,2022 tayari yametajwa na kupelekea mawakili wa CHADEMA kutoa pingamizi dhidi ya maombi hayo ya zuio, ambapo inapinga usikilizwaji wa maombi hayo ikidai kiapo cha kuyaunga mkono kina kasoro za kisheria.