Dk Tulia Ambana Ole Sendeka, Afuta Hoja yake



Dodoma. Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amelazimika kufuta sehemu ya hoja yake bungeni baada ya Spika wa Bunge,  Dk Tulia Ackson kumbana atamke kifungu cha sheria kilichofuta apori tengefu mkoani Manyara.


Sendeka amekutana na mtihani huo leo Jumatatu Juni 20,2022 wakati akichangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2022/23.


“Waziri (Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana) haoni jelaha kwa wafugaji, anatangaza Simanjiro kwa ujumla wake kuwa pori tengefu yaani wilaya nzima ya Longido kwa asilimia 100. Kwa nia ya Pindi Chana sasa itakuwa pori la akiba na sijui wananchi wanaenda wapi,”amesema.


Amesema eneo la Ngorongoro lililobaki linamegwa kwa sura ya kuondoa kilometa za mraba 8,300 na linalobaki kilometa za mraba zisizozidi 2,700.


“Haiwezi kukubalika, ushauri wangu ni kukaa na wananchi Loliondo, wakawashirikisha kwa sababu sheria haziruhusu kuchukua eneo hilo kulifanya tengefu kwa kugeuza ardhi yote ya wamasai kuwa mapori ya akiba,  wanatishwa mzigo wa kujiuliza maana yake ni nini,”amesema.


Hata hivyo, alisimama Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ambaye aliomba kumpa Ole Sendeka taarifa na kusema taarifa ya Dk Chana ilieleza zoezi hilo halitahusisha maeneo ya wananchi.


ADVERTISEMENT

“Kwa hiyo maeneo yanayopandishwa hadhi kutoka maeneo tengefu kuwa mapori ya akiba ni potential (muhimu) kwa uhifadhi na hayana wananchi ndani yake,”amesema.


Alipoulizwa na Dk Tulia kama taarifa hiyo anaikubali, Ole Sendeka alikataa kuipokea taarifa hiyo na Dk Tulia alimtaka kusoma kifungu cha sheria ambacho kilifuta mapori hayo tengefu.


Baada ya kusoma kwa kurudia zaidi ya mara moja, Dk Tulia amesema hakuna kifungu cha sheria ambacho kilifuta maeneo hayo kuwa mapori tengefu na kumtaka mbunge huyo kuchagua kuendelea na hoja hiyo kama anao ushahidi wa kutosha ama kuiondoa.


Katika majibu yake Ole Sendeka amesema yeye si mtaalamu wa mambo ya tafsiri ya kisheria  na kuiondoa hoja hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad