Familia ya Mke na Mume zaungana Katika Msiba




Mwanza. Familia ya Swalha Salum (28) anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mume wake iliungana na familia ya mwenza wake huyo, Said Oswayo kuomboleza kifo cha mwanamume huyo ambaye alijiua kwa kujipiga risasi.

Tofauti na awali, familia hizo ziliomboleza kila moja kivyake vifo vya wapendwa wao, kwa familia ya Swalha kuweka msiba nyumbani kwao eneo la Kirumba, huku familia ya Said ikiweka msiba nyumbani kwake Mtaa wa Mbogamboga eneo la Buswelu.

Hata hivyo, jana familia ya mwanamke iliungana na upande wa mume kuomboleza.

Ushirika wa familia hizo ulianza kuonekana Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando wakati wa kuchukua mwili wa marehemu Said hadi ulipofikishwa nyumbani kwake wilayani Ilemela.


Salum Puva, baba mzazi wa marehemu Swalha ndiye aliyeongoza familia yake katika maombolezo hayo kuanzia hospitalini hadi nyumbani, huku muda wote akiwa amemshikilia mkononi mtoto wa marehemu Said aliyezaa kabla ya ndoa ya wawili hao iliyofungwa Desemba 31 mwaka jana.

Vifo vya wanandoa hao vilitokea usiku wa Mei 28, baada ya Said kumuua kwa kumpiga risasi mkewe Swalha wakiwa nyumbani kwao kisha kujiua yeye mwenyewe kwa risasi pia katika ufukwe wa Rock Beach jijini hapa.

Mwananchi lililokuwa likifuatilia hatua kwa hatua msiba huo, lilimshuhudia Puva akiwa miongoni mwa ndugu upande wa mke waliopanda magari kwenda Kijiji cha Etaro wilayani Musoma kumzika marehemu Said.


Ushirikiano ulioonekana jana huenda ukatuliza hali ya hewa iliyoonekana kutokuwa nzuri kati ya pande hizo mbili tangu mauaji hayo yalipofanyika.

Awali, familia ya Said iliwatuhumu wakwe zao kwa kufunga milango ya nyumba na kuondoka na funguo kiasi cha wao kulazimika kuomboleza wakiwa nje.

Akizungumzia ushirikiano ulioonekana jana, Ally Mchia aliyejitambulisha kuwa ni baba mdogo wa Swalha, alisema msiba uliotokea siyo tu ulikuwa mzito kwa familia zote mbili, bali ni pigo lililowakumba na linahitaji utulivu, uvumilivu na mshikamano kwa pande zote.

“Naamini baada ya kukamilisha taratibu zote za maombolezo, ikiwamo kuwapumzisha wapendwa wetu, familia zetu zitakutana kuzungumzia masuala ya familia,” alisema Ally.


Chambi Lukonga, aliyezungumza kwa niaba ya familia ya Said, aliwashukuru ndugu, jamaa, majirani na marafiki kwa kujitokeza kuungana nao katika hatua zote za maombolezo ya mpendwa wao, huku akiwaomba waendelee kuwaombea kwa Mungu waufikishe salama mwili wa Said na kumzika nyumbani kwao wanakompeleka.

Alisema taarifa za wanandoa hao kufariki kwa kupigwa na kujipiga risasi ziliibua mshtuko kwa sababu ni watu waliokuwa wakiishi kwa amani na upendo.

“Taarifa hizi zimeibua mshtuko na taharuki kwa upande wa mwanamke kama ilivyo kwa upande wetu pia, nawasihi wanafamilia wote kuwa na subra wakati huu wa maombolezo hata baada ya msiba kwa sababu naamini mwafaka utapatikana kwa wote,” alisema Lukonga.

Mwili kutoingizwa ndani

Msafara uliotoka hospitalini ulipofika nyumbani, mwili wa Said haukuingizwa ndani kabla ya kuanza safari ya kwenda Musoma, jambo ambalo Lukonga alisema linatokana na mwili kuharibika kutokana na kukaa ndani ya maji kwa siku mbili na kuwahi kuanza safari ya kwenda Musoma kwa maziko.


“Nawashukuru wakazi wa Mwanza, ndugu, jamaa na marafiki kwa kujitokeza kuungana nasi katika misiba yote miwili ya Swalha na Said. Niwaombe radhi kwamba hatutaingiza mwili ndani, kwa sababu tunataka tuwahi kwenda Musoma kumpumzisha mwenzetu kwa sababu mwili wake umeshaanza kuharibika,” alisema Lukonga.

Alisema familia imepanga maziko kufanyika baada ya kufika kijijini Etaro kulingana na muda watakaowasili.

Ufafanuzi nyumba kufungwa

Hata hivyo, madai ya upande wa mwanamke kufunga nyumba na kuondoka na funguo zilikanushwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Mairi Makori aliyesema nyumba hiyo ilifungwa kwa sababu za kiusalama na kiuchunguzi baada ya tukio.

“Ni kweli baada ya kufunga milango ya nyumba ya marehemu, funguo zote zilikabidhiwa kwa ndugu upande wa mwanamke lakini usiku wa juzi, Mei 31 familia ya mwanaume ilikabidhiwa funguo hizo kwa ajili ya kuendelea na shughuli za msiba,” alisema Makori.

Alitaja sababu nyingine ya nyumba hiyo kufungwa kuwa ni hofu waliyokuwa nayo watu waliokuwa wakiishi nyumbani kwa wanandoa hao, wakiwamo wadogo wa Swalha ambao kwa uoga wa kutojua kikatachotokea baada ya shemeji yao kuondoa akiwa na bastola mkononi waliifunga na kwenda nyumbani kwao Kirumba.


“Lakini baada ya ndugu wa mwanaume kufika walikabidhiwa funguo,” alisema Makori.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad