FAMILIA ya Kibabu Msese (26), mkazi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha aliyefariki katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukamatwa na polisi wilayani humo, imesema haitauzika mwili huo hadi hapo itakapopata majibu ya kilichosababisha kifo cha ndugu yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo.
Akizungumza kwa uchungu nyumbani kwa marehemu, kaka wa marehemu, Petro Msese, alisema jana kuwa wanaiomba serikali kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya ndugu yao huyo aliyedai kauawa kutokana na kipigo cha askari polisi baada ya kukamatwa.
"Sisi familia tumekubaliana hatutazika mwili wa ndugu yetu mpaka tutakapopata majibu ya kina juu ya kilichosababisha kifo chake, kwa sababu mwili unaonekana ameng'olewa kucha za miguu lakini pia amevunjwa shingo," alidai.
Mke wa marehemu, Catherine Jeremia, alisema siku ya tukio mtoto wao mdogo alikuwa mgonjwa ndipo mumewe akamwambia anakwenda kuchukua pikipiki ili wampeleke hospitalini lakini ghafla alishangaa kumwona mume wake amerudi akiwa ndani ya gari la polisi.
Alidai kuwa baada ya kuona gari la polisi, alipigwa na butwaa na kuuliza 'kuna tatizo gani?' na kujibiwa na mmoja wa askari hao waliokuwa na silaha kwamba asiwe na wasiwasi, angejua kilichowapeleka polisi huko nyumbani kwake.
"Walifanya ukaguzi kila mahali ndani ya nyumba, hawakupata chochote. Wakakagua kwa kupanda juu ya dari la nyumba ambapo hawakupata kitu kisha wakakagua chooni na jikoni bila kupata chochote," alisimulia.
Mjane huyo alidai kuwa baada ya kukosa vitu walivyovitaka, askari polisi hao waliketi sebuleni kisha wakadai stakabadhi ya simu yake ya kiganjani na 'sabufa' na kwamba mumewe aliwapatia na baadaye waliamua kuchukua kiambaza (screen) na kuondoka nacho.
Mjane huyo aliyesimulia mkasa huo huku mara kadhaa akikatishwa na hisia za msiba na kuhamia kwenye kilio, alidai aliandaa chakula na kukipeleka Kituo cha Polisi Karatu lakini mumewe aliyekuwa mahabusu huko alipoitwa hakuitika, na kwamba askari polisi aliyekuwa zamu alimtaka mjane huyo aondoke kwa madai kuwa angemwona mumewe siku iliyokuwa inafuata.
"Nilifika nyumbani nikamweleza shemeji yangu kuwa sikufanikiwa kumwona mume wangu ili apewe chakula lakini aliniambia atakwenda mwenyewe siku itayofuata na alipofika kituoni, aliambiwa kuwa ndugu yake aliugua ghafla na kupelekwa hospitalini hapa hapa Karatu," alidai.
Alisema baada ya kufika hospitali waliambiwa kuwa ndugu yao alikuwa amepelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) baada ya hali yake kuwa mbaya na walipokwenda hospitalini, walikuta ameshafariki dunia.
"Ninaomba serikali inisaidie haki ya marehemu mume wangu ipatikane kwa sababu kifo chake kina utata mkubwa na ameniacha na watoto wawili ambao bado walikuwa wanahitaji malezi bora ya baba yao," alisema.
KAULI YA POLISI
Hata hivyo, akizungumza jana jijini Arusha na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alidai mtuhumiwa huyo alifariki dunia Mei 31, mwaka huu kwenye hospitali hiyo na kwamba alikuwa jambazi.
Alisema taarifa za awali zinaonyesha kijana huyo alikamatwa na wengine wanne (hakutaja majina yao) kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha Mei 11 mwaka huu usiku katika eneo la Manyara Kibaoni wilayani Karatu.
"Hawa watuhumiwa walienda kuvamia duka la M-pesa la mfanyabiasha Innocent Olotu na mkazi wa hapo Kibaoni na kupora zaidi ya Sh. milioni 14.5, simu janja na mashine za uwakala wa benki," alidai.