Dar es Salaam. Wakati takwimu mbalimbali zikionyesha mimba shuleni, vyuoni zikipungua, Mwananchi limebaini kuzuka kwa mbinu mpya haramu za utoaji mimba ambapo dawa zilizotengenezwa maalumu kutibu magonjwa ya aina fulani, ndizo zinazotumika kinyume kufanikisha vitendo hivyo.
Hatua hiyo inakuja kutokana na baadhi ya maduka ya dawa hivi sasa kutaka vyeti vya daktari ili kuuza dawa za kutolea mimba, Misoprostol na dawa za dharura za kuzuia ujauzito ‘Emergence Contraceptive Pills’ maarufu P2, waathiriwa wa mimba zisizotarajiwa sasa wamegeukia vidonge vya flagyl (metronidazole).
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini wasichana hao wamekuwa wakimeza tembe nne mpaka nane ili kutekeleza azma hiyo, hali inayowaweka hatarini kupata vifo vya ghafla, magonjwa ya ini na figo.
Alipotafutwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale kuzungumzia sakata hilo alisema flagyl ni aina ya antibaotiki na hazikutengenezwa kutoa mimba.
“Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo chini ya mpango wa One Health, tunafuatilia mpango wa matumizi ya dawa za antibiotiki ili kuzuia usugu wa dawa.
“Nawasihi wananchi kutotumia dawa hizi bila kuandikiwa na daktari, kwani matumizi holela ya dawa hizi yanasababisha usugu wa dawa ambao ni gharama kubwa sana kwa mgonjwa mwenyewe na Serikali kwa ujumla wake,” alisema Dk Sichwale.
Wakati Serikali ikitoa msimamo huo, utoaji mimba ni kosa kisheria kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Kanuni za adhabu Sura Namba 16, kwenye kifungu namba 150, kifungu kidogo namba 2, kutoka aya (B); kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa kujaribu kutoa mimba.
Pia sheria hiyohiyo kifungu namba 150, kinatoa adhabu ya miaka saba jela kwa mwanamke ambaye atakula sumu au kitu chochote na kusababisha mimba kuharibika.
Ripoti ya hali ya idadi ya watu duniani mwaka 2022, iliyotolewa Machi 30 na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na idadi ya watu na afya ya uzazi (UNFPA) linasema karibu nusu ya mimba zote, ambazo ni milioni 121 kila mwaka duniani kote, hazikutarajiwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya mimba zisizotarajiwa huishia katika utoaji mimba na inakadiriwa asilimia 45 hutolewa katika njia zisizo salama ambapo husababisha asilimia 5 mpaka 13 ya vifo vya uzazi.
Inavyotumika
Dawa hiyo iliyo maalumu kutibu mchafuko wa tumbo ikiwemo kuharisha, kutibu maambukizi ya protozoa, kusafisha kizazi baada ya kujifungua au mimba kuharibika kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kundi la wasichana hasa wanafunzi wa vyuo wamekuwa wakiitumia kinyume kuzuia mimba isitunge na kutolea mimba.
Mmoja wa wanafunzi kutoka chuo kimoja jijini Dar es Salaam (jina limehifadhiwa) alisema ameshawahi kumuona rafiki yake wa karibu anatumia flagyl na alipomuuliza inasaidia nini aliambiwa kuwa huzuia mimba.
“Rafiki yangu alinieleza kuwa dawa hii unaitumia baada ya kufanya tendo la ndoa kwani inasaidia kuzuia mimba kama ulikuwa katika siku ya hatari,” alisema
Hata hivyo, Mwananchi lilimhoji mwanafunzi mwingine anayesoma Shahada ya Mawasiliano ya Umma (jina limehifadhiwa) yeye alisema ameshawahi kutumia dawa ya Flagyl kwa kumeza vidonge kadhaa kwa wakati mmoja pamoja na kunywa maji mengi.
“Baada ya kufanya tendo la ndoa wakati nikijua nipo katika siku za hatari nilisubiri baada ya saa 24 ndipo nilipoanza kutumia dawa hiyo kwa ajili ya kuzuia nisipate mimba,” alisema.
Janeth Johnson (si jina halisi) kutoka katika Chuo kimoja jijini Mwanza alisema wakati yupo mwaka wa kwanza alipata ujauzito. “Siku moja nikiwa katika vimbweta vya chuo alikuja rafiki yangu niliyemueleza changamoto niliyokuwa nayo akanipa flagyl ili niweze kutoa ujauzito, nakumbuka aliniambia ujauzito utaharibika na hautakuwa na mimba tena, nilimeza mimba ikaharibika,” alisema.
Evance Mdoe (si jina halisi) aliliambia gazeti la Mwananchi alishawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwenza wake alikuwa anamshangaza, kwani kila baada ya kumaliza tendo alimwagiza amtafutie flagyl ili aitumie.
“Siku moja nilimuuliza, kwani hii dawa kazi yake ni nini, ndipo aliponiambia kuwa inazuia mimba,” alisema Mdoe.
Hata hivyo, baadhi ya wasichana vyuoni wanaamini kuwa flagyl ni dawa ambayo kazi yake ni kuzuia na kutoa mimba na si kwa ajili ya kutibu vimelea mbalimbali kama inavyojulikana.
Wataalamu
Daktari wa binadamu, Shita Samweli alisema dawa ya Fragyl inatumika kutibu uvamizi wa maambukizi ya protozoa kama vile amoeba, kutibu uambukizi wa bakteria wanaoshambulia eneo la utumbo mpana na wanaoonekana kwa njia ya kujamiiana.
“Kuitumia kuzuia mimba ni matumizi holela ya dawa, uvumi huu wa dawa hii kusaidia kuzuia mimba na kutoa mimba haujaanza leo,” alisema Dk Shita.
Vilevile dawa hii kabla ya kupatikana dawa madhubuti, imewahi kutumika miaka ya nyuma kama kutibu malaria na minyoo, hivyo basi hapa tunapata picha kuwa dawa hii si sawa kuitumia kama dawa ya uzazi wa mpango.
Dk Rachel Mwinuka alisema Flagyl inatumika kutibu magonjwa yanayosababishwa na bakteria mwilini na kazi yake kubwa ni kuua vijidudu vya bakteria mfano magonjwa kama UTI, bakteria wa vidonda vya tumbo na kadhalika.
“Flagyl haizuii mimba, yenyewe huwa inaharibu mimba na katika kuharibu mimba watu wanazidisha dozi,” alisema Dk Mwinuka.
Angalizo la wafamasia
Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba alisema kisayansi dawa ya flagyl ina kiambata hai cha metronidazole ambacho kinafanya dawa hiyo isiwe na madhara makubwa kwenye mimba, ingawa haishauriwi mjamzito aitumie.
Alisema Flagyl ni moja ya dawa zisizo salama kutumika kwenye ujauzito, hasa miezi mitatu ya mwanzo kwani zitamsababishia madhara mhusika lakini pia dawa nyingine hazipaswi kutumika pasi ushauri wa mtaalamu.
“Flagyl haina uwezo wa kuweza kuisukuma mimba ikatoka, haina uhusiano moja kwa moja kwamba inaathiri mji wa mimba ikasababisha kutoka kama ilivyo kwa Miso na nyinginezo.
“Ndiyo maana wanameza vidonge vingi kwa maana dawa yoyote iwapo ukaitumia kupita kiasi inaweza kuleta shida kama ni ujauzito ambao upo miezi mitatu ya mwanzo utatoka, ndiyo maana tunawalinda wajawazito wasizitumie kuna dawa nyingine mbadala wanatumia,” alisema Mnyemba.
Mfamasia Wilbard Steven kutoka Baraza la Famasia yeye alisema flagyl sio dawa maalumu kwa ajili ya kutoa mimba kwani ni Antibiotiki na hutumika mara nyingi kama dawa ya tumbo.
Utafiti
Utafiti uliofanywa na watafiti kutoka taasisi ya Guttmacher iliyoko Marekani, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), waligundua makadirio ya mimba 405,000 zilitolewa nchini ndani ya mwaka 2013.
Nyingi kati ya mimba hizo hutolewa kwa taratibu zisizo salama na kuhatarisha maisha ya wanawake.