Papa Francis (85), amelazimika kuahirisha safari yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Sudan Kusini, iliyopangwa kufanyika Julai 2 hadi 7, 2022 kutokana na maumivu ya goti yanayomkabili.
Mkurugenzi wa Shirika la Ofisi ya Waandishi wa Habari la Holy See, Matteo Bruni amesema taarifa hiyo inatolewa baada ya kikao kilichofanyika Makao makuu Vatican, na kwamba tayari wamezitaarifu nchi hizo mbili juu ya kuahirishwa kwa ziara hiyo.
“Baba Mtakatifu, alikubali ombi la madaktari wake na ili kutoathiri matokeo ya matibabu ya goti ambayo bado yanaendelea, analazimika kuahirisha safari yake hadi itakapotangazwa hapo baadaye,” amesema Bruni.
Tangazo hilo ambalo halikutarajiwa, linakuja wakati ambapo tayari maandalizi ya mapokezi yalikuwa yamefanywa na Vatican ikiwa imezindua mpango wa safari hiyo ya siku sita ya Papa kuzuru jijini Kinshasa, Goma na Juba nchini Somalia.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikutaja safari ya Papa ya nchini Canada, iliyopangwa kufanyika July 24 hadi 30, 2022, na alitarajiwa kuomba upya msamaha wa unyanyasaji katika shule za makazi kwa watu wa kiasili aliofanya miongo kadhaa.
Mapema mwezi wa Mei, Lebanon ilitangaza kuahirishwa kwa ziara ya Papa nchini humo iliyopangwa kufanyika mwezi wa Juni, kwa madai kama hayo kuwa alikuwa hayupo imara kiafya.
“Papa ana maumivu makali katika goti lake la kulia, na amekuwa kwenye kiti cha magurudumu tangu mwanzoni mwa mwezi Mei akisema atalazimika kudungwa sindano za dawa za kuzuia maumivu,” alifafanua Mkurugenzi Bruni.
Hata hivyo, Papa mwenyewe anasema “Nimekuwa katika hali hii kwa muda sasa, siwezi kutembea tena,” aliambia gazeti la kila siku la Italia la Il Corriere della Sera, baada ya kulazimishwa kughairi mikutano kadhaa iliyopangwa katika ajenda yake.
Aidha, inadaiwa kuwa pia Papa anaugua maumivu ya nyonga ambayo yanamfanya akose nguvu, na itakumbukwa kuwa Julai 2021 alifanyiwa upasuaji na kupumzishwa kwa siku kadhaa