HESLB Yaanza Kuwadai Shilingi 10.6 Bilioni Waliokopeshwa Law School Of Tanzania


 

HESLB imesaini mkataba wa makubaliano na Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania), kuanza kudai wanasheria walionufaika na  mikopo, Juni 21,2022.

Wanasheria 5,025 waliokopeshwa zaidi ya Shilingi Bilioni 10.6 kama mikopo wakiwa wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya uanasheria Tanzania Tanzania (Law School of Tanzania -LST) watapaswa kurejesha mikopo hiyo kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).


Akizungumza wakati wakisaini mkataba wa makubaliano hayo  Juni 21, 2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw.Abdul-Razaq Badru amesema kuwa Bodi hiyo imekuwa na uzoefu na utayari wa kutekeleza jukumu hilo na kuwakumbusha wanufaika hao kujitokeza na kurejesha.


“Tumejipanga kuanza kuwahudumia kuanzia Julai 1,2022 hivyo tunatoa wito kwa wateja wetu hawa kurejesha fedha hizi pamoja na zile walizokopeshwa wakiwa wanafunzi wa shahada za kwanza ili ziwanufaishe vijana wengine wa kitanzania wanaohitaji”. Amesema Bw.Badru.


Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) Jaji Dkt. Benhajj Masoud amesema wanasheria hao ni wale walionufaika na mikopo ya elimu wakiwa wanafunzi wa LST kati ya mwaka 2008 na 2015 wakisoma Stashahada ya Juu ya Uanasheria kwa Vitendo (Post Graduate Diploma in Legal Practice) wakati Sheria ya HESLB ilipokuwa hairuhusu wanafunzi wa LST kukopeshwa.


“Tunashukuru kuwa mikataba waliosaini walipokuwa wanafunzi -wanasheria ipo wazi kuwa LST inaweza kuipa kazi ya kukusanya madeni haya taasisi yoyote ya umma au binafsi  na hivyo basi baada ya mazungumzo tangu 2019, leo tumefikia hatua hii”. Amesema Jaji Dkt.Benhajj Masoud


HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa elimu ya juu na pia kukusanya fedha za mikopo zilizoiva ambazo zimetolewa na Serikali kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu tangu mwaka 1994/1995

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad