RAFIKI yangu Pablo Martin Franco hajatimiza mwaka tangu awasili nchini. Lakini sasa ameshaondoka. Alikuja na begi dogo Novemba 9, mwaka jana. Nadhani alijua kwamba huenda asiwepo nchini kufikia Novemba 9 ya mwaka huu.
Alianza kwa kujichongea kwamba aliwahi kufundisha Real Madrid akiwa kocha msaidizi chini ya Zinedine Zidane. Tulipopekua mafaili hatukuona jina lake zaidi ya kukutana na picha yake akiwa amepiga na Zidane katika uzio ambao unawatenganisha mashabiki na timu. Nadhani alipiga kama shabiki.
Tuachane na hayo. Kwanini Pablo ameondoka? Ni swali pana. Lina majibu mengi katika soka la kisasa. Kwa mfano, inawezekana mkataba wa Pablo ulikuwa umemuelekeza kwamba asipoifikisha timu hatua ya nusu fainali michuano yoyote ya Afrika basi anaondolewa.
Haya ndio malengo rahisi ya kuamua kuachana na kocha au kuendelea kuwa naye. Ni malengo ambayo yanawekwa na klabu kwa ajili ya kulinda maslahi ya klabu. Wakati mwingine kocha anaweza asifikie malengo lakini ghafla timu ikacheza kandanda safi na ikaamua kuendelea naye.
Makocha wa aina ya Pablo wapo wengi duniani. Inasemwa kwamba duniani kuna makocha wengi zaidi wasio na kazi kuliko wale walio kazini. Inapotokea kazi ya namna hii ni rahisi kwa makocha wa hadhi ya Pablo kujipatia kibarua kwa gharama yoyote ile, hata kwa mkataba wa namna hii.
Kwa hiyo inawezekana kabisa Pablo amekubali kilichotokea kwa urahisi kwa sababu hakufikia malengo. Bahati mbaya kwake umekuwa ni msimu wenye mambo mengi katika Simba kiasi kwamba ni vigumu kujua kama tatizo alikuwa yeye au mambo mengine.
Pablo alikuwa wakati Simba ikiwa imemuondoa Didier Gomes kwa sababu kama yake. Lakini ni katika msimu huu Pablo alikuwa anasimuliwa tu uhodari wa Simba iliyopita ya kina Clatous Chama na Louis Miquissone. Hakuwakuta.
Ni katika msimu huu Pablo alikuja kukutana na wachezaji wapya ambao mpaka sasa wamegawanya hisia za mashabiki. Je timu yao ilipatia usajili au haikupatia? Wamefaulu kwa Sadio Kanoute au ni mchezaji wa kawaida? Vipi kwa Ousmane Sakho? Leo anacheza hivi kesho anacheza vile.
Vipi kwa kina Jimmyson Mwinuke? Kibu Dennis? Yusuph Mhilu? Sidhani kama mashabiki wa Simba wana uhakika kuwa mastaa hawa wameweza kuziba viatu vya Miquissone. Vipi Rally Bwalya alijitahidi kuziba pengo la Chama wakati hayupo? Sidhani.
Kuna mgawanyiko wa hisia ingawa ni rahisi kwa wachezaji kupona. Wachezaji ni wengi kwa hiyo huwa hawafukuzwi. Lakini kocha anabeba lawama zao. Kuna wachezaji wengi watapona lakini ukitazama nyuma unajua kwamba kuna mahala halikuwa tatizo la kocha.
Hapo hapo ulikuwa ni msimu ambao kulikuwa na wachezaji wengi muhimu waliokaa nje kwa sababu ya majeraha. Tazama pambano la Simba na Yanga nusu fainali za Shirikisho pale CCM Kirumba jinsi ambavyo Simba ilikuwa hoi. Jukwaani nilikuwa nimekaa na Shomari Kapombe na msaidizi wake, Israel Mwenda. Walinzi wawili chaguo la kwanza upande wa kulia walikuwa jukwaani. Uwanjani alikuwa anacheza Jimson Mwanuke ambaye ni winga. Alijitahidi kwa kiasi chake. Jukwaani pia alikuwepo John Bocco, lakini Aishi Manula alikuwa katika benchi akimtazama Beno Kakolanya akicheza. Mwamba wa Lusaka alikuwa kwao Lusaka katika maadhimisho ya kumbukumbu kifo cha mkewe. Jonas Mkude hakuwepo Mwanza. Ilikuwa ni kielelezo cha namna ambavyo msimu ulikuwa umekwenda.
Wachezaji waliojitokeza kuwa muhimu nao muda mwingi walikuwa hospitali. Kwa nyakati tofauti kina Hassan Dilunga, Kibu Dennis, John Bocco, Kanoute, Tadeo Lwanga, Mkude na wengineo wengi wamepitia katika kitanda cha hospitali.
Pengine lilikuwa ni jukumu la kocha kuunganisha timu ya namna hii. Labda ni hapo alipofeli lakini kiukweli ni kwamba Pablo hakufeli sana. Simba itamaliza msimu ikiwa ya pili, imefika nusu fainali michuano ya FA na imefika robo fainali michuano ya Shirikisho.
Kwa viwango ambavyo tumejiwekea wenyewe bado kocha wa namna hii amefeli. Kwa viwango vya Simba yenyewe ni kwamba amefeli. Lakini zaidi ni kwamba amefeli kwa sababu wapinzani wao Yanga wanaonekana kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara na FA.
Zaidi ni kwamba Pablo hajawahi kuifunga Yanga, lakini pia alikuwa amefungwa na Yanga katika pambano la Mwanza. Nilijua kwamba mwisho wake ulikuwa umekaribia. Asingeweza kupona na angekuwa mtu wa kwanza kutolewa kafara. Zaidi ya yote ni kwamba soka la Afrika halina mambo ya programu. Aliletwa kwa ajili ya kazi fulani, akaikubali, ameshindwa, amefukuzwa. Ni tofauti na hao kina Mikel Arteta ambao huwa wanapewa kazi ya kuijenga timu taratibu.
Ni tofauti na kina Jurgen Klopp na Pep Guardiola ambao wamepewa muda wa kujenga vikosi vyao katika utaratibu. Ukiangalia kikosi cha kwanza cha Guardiola wakati anatua City na kikosi chake cha leo ni vitu tofauti. Vivyo hivyo kwa Klopp. Vivyo hivyo kwa Arteta ambaye ameanza kuwaondoa kina Mesut Ozil, Pierre-Emerick Aubameyang, Saed Kolasinac na wengineo huku akijenga timu anayoitaka yeye.
Mpira wa Afrika haupo hivyo. Kocha anakabidhiwa wachezaji wa kufanya nao kazi na lazima hiyo kazi aifanye. Sio kwa Simba tu, bali kwa timu zote za Afrika hasa zile ambazo zina ubavu wa kifedha. Kocha huwa anavumiliwa katika timu maskini tu.
Anachoweza kushauri kocha ni nafasi tu anazohitaji kikosini au aina gani ya wachezaji lakini sio wachezaji wenyewe. Maskini Pablo hakupewa hata nafasi hiyo katika msimu ambao ungekuwa wa pili kwake. Alikuja katika msimu wake wa kwanza huku Simba ikiwa imecheza mechi kadhaa na anaondoka huku Simba ikiwa imebakiza mechi kadhaa.
Hatujaweza kujua ubora wake katika mambo mengine kama vile kuandaa timu yake mwanzo wa msimu na pia kutengeneza timu ya muda mrefu.
Pia hatukujua kwamba alihitaji muda mrefu kidogo kuzoea soka la Afrika na mazingira ya Afrika kwa sababu ilikuwa mara yake ya kwanza kufundisha soka Afrika. Mambo hayo Afrika hayapo na nadhani mwenyewe alifahamu na ndio maana alikuja na begi dogo.
Inawezekana alishasoma mazingira ya soka la Afrika na aina ya mkataba wake. Kila la heri kwake inawezekana huu ukawa mwanzo wa safari yake ndefu katika soka la Afrika.