Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekutana leo Ikulu Chamwino, Dodoma kwa kikao cha siku moja cha kawaida kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM amesema “Pamoja na mambo mengine Halmashauri kwa kauli moja imekubaliana kuwa kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya, CCM imekubaliana na umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hivyo kinaishauri Serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya Watanzania wote”
“Halmashauri Kuu pia imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini kwa lengo la kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa Watanzania wote.
“Halmashauri kuu imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo, Chama kimeishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote, miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini”