NADHANI Stephane Aziz Ki amesaini mkataba na klabu ya Yanga. Juzi nchi ilisimama kidogo kutokana na sakata lake la uhamisho. Huwa inachekesha sana wakati nchi ya Tanzania inaposimama kwa ajili ya mchezaji mmoja tu. Na katika zama hizi za mitandao mioyo ya mashabiki inadunda zaidi.
Ki alicheza mechi mbili dhidi ya Simba akiwa na jezi ya ASEC Mimosas. Kiwango chake kilikuwa cha hali ya juu kwa mujibu wa soka la Afrika. Baada ya hapo Simba na Yanga zikaanza kumfukuzia. Majuzi inadaiwa kwamba Yanga wamemalizana naye rasmi.
Usajili wa Ki umenikumbusha mambo mengi. Kitu cha kwanza umenikumbusha namna ambavyo nyakati nyingine taifa la Tanzania huwa linasimama kupisha ugomvi wa mchezaji mmoja baina ya Simba na Yanga. Huwa imetokea mara nyingi kwa sababu mara mbalimbali.
Sababu ya kwanza huwa ni kama hivi. Mchezaji anapotakiwa na klabu zote mbili kwa nguvu kubwa. Imewahi kutokea kwa wachezaji wa ndani na wa nje. Imewahi kutokea mara nyingi. Mfano wa karibuni ni kama wa Djuma Shaban.
Sababu nyingine ni pale mchezaji anapokuwa amesaini katika fomu au mikataba ya timu zote mbili. Iliwahi kutokea miaka ya zamani halafu ikasogea hapo miaka ya katikati wakati kina, Abubakar Kombo walipofanya hivyo, kisa kina Pius Buswita na wengineo.
Katika haya huwa inachekesha pale unapodhani kwamba mchezaji mwenyewe ni malaika. Kwamba anakuja na suluhisho la matatizo yote klabuni. Kwamba unaweza kudhani anayegombewa ni miongoni mwa wachezaji bora duniani. Zamani nilikuwa nachukia sana. Siku hizi nimejifunza kitu.
Nimejifunza kwamba ni sehemu ya chachu ya ushabiki wenyewe. Ni sehemu ambayo inazifanya Simba na Yanga ziendelee kuwa tamu kwa mashabiki wa soka. Nimekuwa najiuliza kama Gor Mahia na AFC Leopards zinaweza kufanya hivi kwa mchezaji fulani. Nimegundua kwamba huenda haziwezi kwa sababu mbili.
Kwanza kabisa hazina pesa. Lakini pili hazina upinzani huu kwa sasa. Ni upinzani wenye afya kwa hamasa ya soka hata kama mchezaji mwenyewe sio malaika. Ni kitu ambacho majirani zetu wamepoteza. Ni kitu ambacho si ajabu wangetamani kuwa nacho katika njia zote mbili. Njia ya uwezo wa kipesa au hamasa. Hawana zote.
Nje ya jambo hili chanya kuna jambo jingine hasi. Vita ya mchezaji kama Aziz Ki inatokana na ukosefu wa mipango wa klabu zetu. Kwamba Aziz Ki asingegombewa hapa nchini kama asingecheza mechi mbili za ASEC Mimosas dhidi ya Simba. Ina maana kusingekuwa na utaratibu wa kumuona Aziz Ki nje ya hizo mechi.
Hili suala huwa tunalizungumzia kila siku. Suala la kuskauti. Huwa tunapata wachezaji pindi wanapocheza na sisi tu. Ni bahati kuwapata kina Jose Luis Miquissone. Wakati mwingine unaweza kuangukia kuwapata kina Perfect Chikwende.
Kwa mfano, kama ASEC asingekuwa katika kundi la Simba kwanini tusimtazame Aziz Ki akicheza katika pambano kati ya ASEC dhidi ya Horoya ambalo halituhusu? Kwanini isiwe hivyo? Hivi tunajua kuna kina Aziz Ki wangapi kwingineko? Kwanini tumgombee mchezaji mmoja?
Nakukumbusha tu kwamba hata Miquissone alitakiwa na Yanga. Kisa? Walimuona katika mechi mbili ambazo UD Songo ilicheza na Simba. Hawakuwa wamemuona kokote kwingine. Ndivyo mpira wetu ulivyo. Watani huwa wanagongana kwa staili hii kwa miaka yote.
Kumbuka namna ambavyo Chikwende alizigonganisha Simba na Azam hewani. Ni kwa sababu hata Azam walimuona katika mechi mbili alizocheza dhidi ya Simba akiwa katika klabu yake ya Platinum ya Zimbabwe. Hakukuwa na mchezaji mwingine hatari wa nafasi ya Chikwende nje ya klabu yake?
Na achilia mbali suala la kumuona mchezaji ambaye amecheza dhidi ya timu ya Tanzania, nadhani pia huwa tunapenda pia kumchukua mchezaji ambaye ameonyesha uwezo wake akiwa katika jezi ya watani au wapinzani wetu hapa hapa.
Naweza kukutajia wachezaji 20 ambao wamewahi kucheza Simba na Yanga na Azam. Au Simba na Azam. Au Yanga na Azam. Kwa mfano, kwa sasa Simba akili yao inaweza kuwa kumpata Fiston Mayele tu na wala hawatawaza sana kumpata mshambuliaji bora wa Ligi Kuu ya Sierra Leone.
Unashangaa Yanga wanampigia hesabu zaidi, Joash Onyango kuliko wanavyompigia hesabu beki wa kati anayeweza kuwa bora kuliko wote nchini Kenya kwa sasa. Nia yetu ni ile ile. Kuonyeshana ubavu wa pesa pamoja na kukomoana kwa kila njia.
Haishangazi kuona rafiki yangu Aziz Ki ameibuka akiwa shujaa bila ya ushujaa mkubwa. Amewagonganisha wakubwa kichwa kwa sababu ya uvivu wao tu wa kwenda kuchunguza kwingineko. Ingewezekana tu Ki akaenda Simba halafu Yanga ikachukua kiungo bora mchezaji mwingine ambaye ametamba katika makundi mengine ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika.
Labda huu ndio utamu wa Simba na Yanga. Sioni kama mambo haya yanaweza kumalizika kwa sasa. Kama hayakumalizika zamani basi nadhani hayataweza kwisha kwa muda mchache ujao. Dunia ina wachezaji wengi lakini Simba na Yanga zinaweza kuamua kuingia vitani kwa mchezaji ambaye unaweza kudhani ni Lionel Messi.
Rafiki mmoja shabiki wa Simba alinipigia simu akiwa mnyonge kwa sababu Simba imemkosa Aziz Ki. Ungeweza kudhani kwamba dunia haina mchezaji mwingine wa aina ya Aziz Ki. Nani anamjua kiungo bora mchezeshaji wa Ligi Kuu ya Msumbiji? Vipi kuhusu Ghana? Vipi kuhusu Mali?