Kilichowaangusha Kina Mdee na Wenzake Mahakamani Hichi Hapa



MAHAKAMA Kuu Masijala Kuu imeyaondoa maombi ya waliokuwa wanachama 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa yana upungufu mbalimbali wa kisheria.

Wabunge hao 19, wakiongozwa na Halima Mdee, walifungua maombi hayo mahakamani huko kuomba mahakama itoe kibali cha kufungua kesi ya kupinga mchakato uliowavua uanachama wa CHADEMA.

Pia waliomba mahakama iweke zuio la kutokuchukuliwa kwa hatua zozote dhidi yao hadi pale maombi yao ya msingi yatakapoamuliwa. Hadi sasa wabunge hao hawana zuio lolote kutokana na maombi hayo kutupwa.

Uamuzi mdogo huo ulitolewa jana na Jaji John Mgeta baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na mapingamizi saba ya wajibu maombi yaliyotolewa na Wakili Peter Kibatala, ambapo yamekubaliwa mawili na matano yametupiliwa mbali.

Alisema katika maombi hayo, mawili yalikubaliwa na kwamba mahakama imeelekeza wayafanyie marekebisho.


Jaji Mgeta alisema waleta maombi (Mdee na wenzake) walikosea jina la mjibu maombi wa kwanza, walimshtaki mtu ambaye kisheria hayupo, wameishtaki Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA badala ya wadhamini waliosajiliwa (Registered Trustee) kama sheria ilivyoelekeza.

Alisema hiyo ni kwa wa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa kifungu cha 21(1) ambacho kinataka chama chochote cha siasa kikishapata usajili wa kudumu kiwateue na kuwasajili hao trustee kwa mujibu wa sheria ya wadhamini.

Katika mapingamizi ya Kibatala alidai kuwa wakili ana sehemu yake ya kutia saini, kitendo cha mawakili kutia saini katika viapo vya kina Mdee, kina maana wanajimilikisha maelezo ambayo ni ya kuambiwa.


Wakili Jeremia Mtobesya ambaye pia anawakilisha CHADEMA, aliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo ya kina Mdee kwa kuwa wameishtaki Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo haikutakiwa kushtakiwa katika shauri hilo.

Alidai NEC haikutakiwa kuunganishwa katika shauri hilo kwa kuwa mahakama haina mamlaka kisheria ya kuhoji uamuzi wake kwa mujibu wa ibara ya 74 (12) ya Katiba ya nchi.

Akijibu hoja za pingamizi hilo, Wakili Aliko Mwamanenge kwa niaba ya Halima Mdee na wenzake, aliiomba mahakama itupilie mbali mapingamizi hayo kwa sababu hoja zao hazina msingi wowote.

Alidai kuwa katika kesi hiyo, NEC bado haijataja majina au kuchagua wabunge wengine wa kujaza nafasi za kina Mdee, bali waleta maombi wanachotaka kuzuia NEC kufanya chochote.


Wakili Ebson Kilatu wa upande wa waleta maombi, akijibu hoja ya kuishitaki Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA, alidai ni sahihi kuishitaki kwa kuwa ndicho chombo kinachofanya uamuzi wa chama.

Kuhusu hoja ya mawakili kutia saini katika viapo hivyo, Wakili Kilatu alidai hawajatia saini katika viapo hivyo, bali waliandika tarehe ya uandaaji viapo hivyo na kutia saini eneo hilo ambalo haiathiri hoja za maombi hayo.

NJE YA MAHAKAMA

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alipongeza alichokiita haki kutendeka, imeshinda udhalimu, dhuluma na usaliti, hivyo kutokana na uamuzi huo, mara moja Wakili Mkuu wa Serikali atapaswa kupeleka taarifa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na yeye ataipeleka kwa Spika wa Bunge ili kina Mdee waondolewe bungeni.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, alisema ni tukio la kihistoria kwa CHADEMA kwa kuwa walikuwa hawajawahi kuwavua uanachama wabunge 19.


“Tunategemea kuwa Spika wa Bunge (Dk. Tulia Ackson), ataijulisha rasmi NEC kuhusu nafasi 19 kuwa wazi baada ya Mahakama Kuu kutupa kesi yao na hivyo ni rasmi wamepoteza haki ya kuendelea kuwa wabunge, Spika anawajibika kutimiza matakwa ya Katiba ya nchi," alisema.

*Imeandikwa na Grace Gurisha na Romana Mallya


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad