Kina Mdee Wawasilisha Mahakakani Sababu Tano Kuishtaki Chadema




Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema akiwa na Katibu wake, John Mnyika katika mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
WABUNGE viti maalum 19, wakiongozwa na Halima Mdee, wamewasilisha Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, sababu tano za kuomba ikubali maombi yao ya kufungua kesi kupinga kufukuzwa Chadema. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Sabahu hizo zimewasilishwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Mustafa Ismail, Leo Alhamisi, tarehe 30 Juni 2022, na mawakili wa kina Mdee, wakiongozwa na Wakili Ipilinga Panya.

Wakili Panya ametaja baadhi ya sababu hizo, ikiwemo waleta maombi kuwa na maslahi katika kesi hiyo, wakati nyingine ikiwa ni muda.

Wakili Panya amedai, kina Mdee Wana maslahi na kesi hiyo kwa kuwa wameathirika na maamuzi ya mjibu maombi wa kwanza, Baraza la Wadhamini la Chadema, kufuatia uamuzi wa Baraza Kuu lake, kuwafukuza uanachama bila kufuata utaratibu.


Amedai, wabunge hao waliteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa udhamini wa chama cha Chadema.




“Wao ni wabunge viti maalum walioteuliwa na NEC kwa udhamini wa Chadema tangu Novemba 2020. Maamuzi ya Baraza Kuu ya tarehe 11 Novemba 2022 ya kuwafukuza uanachama bila kufuata utaratibu na kusikilizwa kama inavyooneshwa kwenye kiapo cha kila mleta maombi, yanawagusa kama wanachama wa chama cha siasa na wabunge,” amedai Wakili Panya.

Kuhusu sababu ya muda, Wakili Panya ameiomba mahakama hiyo ikubali ombi la kina Mdee kufungua kesi ya kupinga kufukuzwa Chadema, kwa kuwa maombi yao yamewasilishwa mahakamani ndani ya muda wa kisheria.


Naye wakili Aliko Mwamanenge, ametaja sababu nyingine za kina Mdee kuomba maombi yao yakubaliwe, kuwa kesi hiyo siyo ya kubishaniwa.

Wakili Mwamanenge amedai kuwa, kuna baadhi ya hoja katika maombi hayo hayajapingwa na upande wa wajibu maombi, ikiwemo Kamati Kuu ya Chadema, kutoa uamuzi wa upande mmoja kwani kina Mdee hawakusikilizwa.

Wakili huyo wa kina Mdee, amedai wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, waliotoa uamuzi wa kuwafukuza uanachama tarehe 26 Novemba 2020, ndiyo hao walioshiriki katika kikao cha Baraza Kuu, kilichotupilia mbali rufaa zao za kupinga kuvuliwa uanachama.

Baada ya Wakili Mwamanenge kumaliza kuwasilisha sababu hizo, Jaji Ismail ameahirisha Kesi hiyo kwa muda wa saa moja , ambapo ikirejea mawakili wengine wa kina Mdee wataendelea kuwasilisha hoja zao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad