Kocha Msaidizi wa Simba Matola Anasikilizia ishu



KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola amesema hatma ya kuendelea kuwepo Msimbazi na kuanza maandalizi ya msimu ujao inategemea na maamuzi ya mabosi wa klabu hiyo, kwani anawasikilizia wakati mkataba wake ukielekea ukingoni.

Matola ambaye amekuwa akitumika kama kocha msaidizi kwa makocha kadhaa wa kigeni wanaokuja na kuondoka Msimbazi na kwa sasa ndiye anayekaimu nafasi ya Pablo Franco kutoka Hispania aliyesitishiwa mkataba wake hivi karibuni.

Akizungumza na Mwanaspoti akitoka kuiongoza Simba kushinda mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City, Matola alisema kwa sasa hajaanza rasmi maandalizi ya msimu ujao kwani bado timu hiyo haijamkabidhi mikoba rasmi ya kuwa kocha mkuu na anawasikilizia viongozi tu ili kuanza kusuka timu kwa msimu ujao.

“Nashukuru kwa nafasi hii niliyopo sasa, tunaenda kujipanga kwa ajili ya mechi zilizobaki ili kuhakikisha tunashinda zote na kumaliza msimu vizuri,” alisema Matola na kuongeza;


“Kuhusu msimu ujao, kuna mambo bado hayajakamilika, yapo kwenye uongozi na yakikamilika basi mtajulishwa nini kinafuata ila sasa muda bado na nasikilizia, kila kitu kikikaa sawa mtaona.”

Matola amehudumu Simba kwa vipindi tofauti akiwa kama mchezaji na sasa kocha ambapo kwa miaka ya hivi karibuni amekuwa kocha msaidizi chini ya makocha tofauti ikiwemo Sven Vandebroeak, Didier Gomes na Pablo ambao wote kwa sasa hawapo na timu hiyo.

Simba ipo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya na siku yeyote kuanzia sasa watamtangaza na taarifa za ndani zinaeleza Matola ataendelea kuwa kocha msaidizi.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad