Kocha Nabi Avutiwa na SIMON Msuva


SIMON Msuva yupo nchini tangu mwaka jana baada ya kuzinguana na timu yake ya Wydad Casablanca ya Morocco na kupelekana Fifa, ila juzi alifunga mabao mawili kwenye mechi ya hisani ya timu Samakiba na kuiwezesha team Kiba kubeba ubingwa wa msimu huu kwa penalti.

Kumbe, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alikuwa akimfuatilia dakika zote za mchezo zilizoisha kwa sare ya mabao 3-3, kisha kupigiana penalti na kuweka wazi kuwa kama kuna jina la mchezaji mzawa limesalia kikosi chake ni Msuva anayetamani awe naye.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema anatamani kuongeza mshambuliaji mmoja mzawa, lakini kiu ni kuwa na staa huyo aliyewahi kukipiga na kung’ara na Yanga kabla ya kutimkia Difaa El Jadida ya Morocco kisha Wydad.

Nabi alisema anatambua Msuva ana mgogoro na mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini kama mabosi wake wanaosimamia usajili watamfungia kazi wanaweza kunasa saini yake.

“Nahitaji mshambuliaji mwenye kujua kufunga na kasi. Nipo hapa Tanzania kuna wakati ni jambo zuri kuendeleza wachezaji wa taifa hili. Natamani sana kufanya kazi na yule Msuva (Simon),” alisema Nabi.

“Msuva ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Napenda sana kasi yake, juhudi zake lakini kitu bora zaidi anaweza kufunga na kucheza nafasi nyingi. Nitafurahi viongozi wangu wakimpata.

“Sisi ni mabingwa sasa hapa Tanzania, tunakwenda kucheza mashindano ambayo kila mchezaji mkubwa angetamani kucheza, kwasasa najua Msuva ana shida na klabu yake, najua yataisha ila wakati huu ni kitu kizuri angekuja hapa Yanga aweze kupambana kujiweka sawa, atalisaidia taifa lake na hata sisi tutapata kitu.”

Nabi alisema anafahamu Msuva ana ndoto za kwenda kucheza soka nje, ila kama atakubaliana na mabosi wa Yanga atamruhusu wakati wowote kwenda kucheza.

“Nilimuona (Msuva) alikuja kwenye vyumba vyetu siku ambayo tuliwafunga Coastal Union. Sote tulifurahia kumuona wachezaji, makocha na viongozi alionyesha kuiheshimu hii klabu na kwamba anatambua alipita hapa na waliishi vizuri,” alisema.

“Kama atakuja hapa tunaweza kumpa mkataba mfupi ambao utamruhusu kuondoka wakati wowote akitaka kuondoka.” Kwa sasa Msuva anajifua na kikosi cha kituo cha soka cha vijana cha Cambiasso baada ya kuwa na mgogoro na timu yake ya Wydad ambao kesi yao ipo Fifa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad