YANGA juzi usiku ilikuwa katika vita vya kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu Bara iliyousotea kwa misimu minne mfululizo mbele ya Simba na siku hiyohiyo wakiwa kwenye Uwanja wa Mkapa kuivaa Coastal Union usiku, Yanga wakapenyezewa ujumbe na wazito wa Shirikisho la Soka la Afrika(CAF) kwamba wakae mkao wa mashindano kwani msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Afrika sasa utaanza Agosti 22. Hivyo ratiba zao waziweke sawa wakati wakiendelea kushangilia ndoo. Achana na matokeo ya mchezo huo wa usiku, hadi kufikia mafanikio hayo, Yanga imepambana kwelikweli chini ya Kocha Nasreddine Nabi.
Baada ya jana, Yanga imesaliwa na michezo mingine mitatu mkononi dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa Juni 22, Mbeya City (Juni 25) na kufunga msimu na Mtibwa Sugar Juni 29.
Siku chache baadaye Yanga itakuwa na kazi nyingine ya kulisaka taji la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Coastal Union katika fainali itakayopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Taji hilo pia lilikuwa likishikiliwa na Simba kabla ya kulitema baada ya kuifunga katika mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo iliyopigwa Mei 28, Uwanja CCM Kirumba, Mwanza.
Mwanaspoti linakuletea ramani nzima ya ubingwa wa Yanga kwa msimu huu ikiwamo rekodi ya kucheza mechi 33 ikiunganisha misimu bila kupoteza, kwani mara ya mwisho kufungwa ilikuwa Aprili 25, mwaka jana (kabla ya mchezo wa jana usiku) ilipovaana na Azam katika mechi ya msimu uliopita.
SIKU 416 ZA KIBABE
Kama hujui tangu Yanga ilipopoteza mechi ya msimu uliopita mbele ya Azam kwa kulala 1-0 kwa bao la shuti kali la mbali la Prince Dube, Yanga haijapoteza mechi yoyote ya ligi kabla ya pambano lao usiku wa jana, ikiwa na maana imetumia siku 416 kibabe bila kuonja uchungu wa kufungwa.
Katika siku hizo 416, Yanga imecheza jumla ya mechi 33 za ligi ikishinda 24, zikiwa tano za mwisho za msimu uliopita na 19 za msimu huu, huku ikitoka sare tisa, zikiwamo mbili za msimu uliopita na saba za msimu huu.
Yanga imefunga jumla ya mabao 53, yakiwamo 42 ya msimu huu na 11 ya msimu uliopita na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 11 ikiwamo saba kwa msimu huu na mbili za msimu uliopita, kuonyesha jamaa walikuwa na siku 416 za kibabe kwelikweli katika Ligi Kuu.
Katika mechi 26 za msimu huu, Yanga imeshindwa kuzifunga timu za Simba nyumbani na ugenini kwa kutoka nao suluhu, Mbeya City ilitoka nao sare nyumbani bado mechi ya ugenini na Namungo ugenini.