Lissu Ampongeza Samia, Atabiri Ujio wa Mabadiliko



MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuanza mazungumzo na chama chake ni kielelezo tosha kwamba nchi inaelekea kwenye Katiba Mpya, mabadiliko makubwa ya kisheria, kitaasisi na muundo mzima wa utawala.

Akizungumza na Nipashe usiku wa kuamkia jana, Lissu alisema anashukuru kwa kulipwa haki yake ambayo ni mafao ya kazi ya ubunge aliyoifanya tangu Novemba 2015 hadi Juni 2019 ilipotangazwa bungeni kwamba amekosa sifa za kuwa mbunge.

Alisema licha ya mafanikio yanayoonekana sasa, bado kuna kazi kubwa ya kuondoa siasa zilizopita ambazo ziliacha majeraha kwa wengi, akiwamo yeye aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana.

“Hiyo inahitaji Katiba Mpya, mabadiliko makubwa ya kisheria na kitaasisi na muundo mzima wa utawala. Kwa kuanza mazungumzo na CHADEMA, Rais Samia ameanza safari ya kuelekea kwenye mabadiliko hayo,” alisisitiza Lissu ambaye amekuwa anaishi Ubelgiji tangu mwaka 2018 alipokwenda kwa matibabu.

Mwaka 2020, Lissu alirejea nchini kwa ajili ya uchaguzi mkuu ambao aliwania kiti cha Rais wa Tanzania, akitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushika nafasi ya pili nyuma ya Dk. John Magufuli (Hayati) aliyetangazwa mshindi.


MADAI YA MATIBABU

Kuhusu hali ya kisiasa, Lissu alisema kuna ahueni kubwa kulinganisha na wakati wa awamu ya tano, lakini bado kuna kazi kubwa ya kuondokana na kabisa na siasa zilizoumiza.

“Nimefurahi kwamba Rais Samia ameanza kurekebisha dhuluma niliyofanyiwa. Bado amebakisha madai yangu ya matibabu na kunihakikishia usalama wangu ili niweze kurudi nyumbani bila kuwa na hofu ya watu wasiojulikana. Natumaini na haya atayafanyia kazi,” Lissu alisema.

Alifafanua: “Ni kweli nimeshalipwa kiinua mgongo changu, bado fedha za matibabu na hizo nimeambiwa niandike barua za kuzidai, na sasa ninakusanya nyaraka zote muhimu kwa kuwa nilitibiwa Nairobi na Ubelgiji."


Lissu, akiwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Septemba 7, 2017, majira ya saa nane mchana, alishambuliwa kwa risasi 32, kati yake 16 zikimpata mwilini, nje ya nyumba yake Area D, Site 3 jijini Dodoma.

Kiongozi huyo alijeruhuwa miguuni na tumboni wakati akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Land Cruiser VX lililopata matundu 25 ya risasi upande alikokuwa ameketi.

Alipatiwa matibabu ya awali kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na baadaye Nairobi, Kenya kisha kuhamishiwa Ubelgiji ambako anaishi hadi sasa na ameshaweka wazi kwamba anaishi na risasi moja mwilini.

Siku chache baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Lissu alidai kutishiwa maisha na kulazimika kuondoka nchini Novemba 10, 2020, akitokea nyumbani kwa Balozi wa Ujerumani, akisindikizwa na Balozi wa nchini na maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).


Februari mwaka huu, Rais Samia akiwa kwenye ziara ya kikazi Ubelgiji, alikutana na Lissu kwa mazungumzo na baadaye mtaalamu huyo wa sheria alibainisha kuwa alimwomba Rais apate hati ya kusafiria ambayo aliipata ndani ya muda mfupi na alipwe stahiki zake.

Katika mazungumzo na Nipashe usiku wa kuamkia jana, Lissu alisema kuwa kabla ya kupatwa na madhila ya kupigwa risasi, alikuwa amekopa kwenye benki kadhaa, mojawapo ilimpeleka mahakamani kwa kuwa hakuwa amelipa mkopo wake kwa muda mrefu.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad