Madudu: Gari la serikali lauzwa mil. 4/-limetembea kilomita




 
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, amemwagiza Katibu Tawala mkoa huo, Missaile Musa, kumwandikia barua aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, mkoani humo kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuuza gari la serikali kwa Shilingi milioni nne.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba.
Mgumba alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki kwenye baraza la kujadili taarifa ya CAG za mwaka 2020/2021 baada ya kuibuka kwa hoja ya gari kununuliwa kwa kiasi hicho cha pesa huku likiwa limetembea kilomita 900 pekee.

Alisema mkurugenzi huyo, Haji Mnasi, alifanya maamuzi ya kuuza gari hilo DFPA yenye namba 8508 aina ya Hilux ambalo halikuwa kwenye orodha ya kuuzwa, na kuuzwa kinyume na utaratibu kwa kutumia nafasi yake ya ukurugenzi.

Pia mkuu huyo wa mkoa alisema, gari hilo mali ya serikali limeuzwa kwa kuiba kadi ya gari kwa mtumishi wa umma ndani ya Wilaya ya Ileje huku akifahamu kuwa ni kosa.

“Katibu Tawala wa Mkoa wasiliana na kamishna ili kupata kadi mpya kwa ajili ya gari hilo ili lirudi kuwa mali ya serikali na kuhakikisha mkurugenzi huyo anarudi kujibu hoja hiyo ili kubaini nini kilimsukuma kuuza gari hilo,” alisema Mgumba.


 
Mkaguzi wa Nje Mkoa wa Songwe, Chausiku Maro, alisema gari hilo lililetwa na serikali kwa ajili ya matumizi ya mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo na kuuzwa kumesababisha mkaguzi huyo kushindwa kufika kwa wakati kwenye miradi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.

“Kama wakaguzi wa nje tumeibua hoja ya kuuzwa kwa gari hilo bila kuwapo kwa nyaraka za vikao halali vya maamuzi na kushauri viongozi wa serikali kuacha kufanya maamuzi kama hayo wakitumia nafasi zao, wanauza mali ya umma kwa masilahi yao wenyewe,” alisema Maro.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya, alisema watahakikisha wanakuwa bega kwa bega kuhakikisha mali za serikali zinatunzwa na kutumika kwa matumizi yaliyopangwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ileje, Ubatizo Songa, alisema utaratibu uliotumika kuuza gari hiyo bila kibali cha baraza la madiwani, vikao vya wakuu wa idara, vikao vya kamati ya fedha haukuwa sahihi.

Diwani wa Kata ya Ibaba, Tata Kibona alisema gari hilo liliuzwa bila maamuzi ya vikao halali, huku akisema lilikuwa maalumu kwa ajili ya matumizi ya mkaguzi wa ndani.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad