Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, imeelezwa jinsi Sh5.3 bilioni za benki ya NBC tawi la Moshi zilivyoporwa chini ya mtutu wa bunduki na kundi la wahalifu takribani 15 walililoingia ndani ya benki hiyo wakijifanya wateja.
Hayo yalijitokeza wakati upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Grace Kabu, alipomsomea maelezo ya awali mshtakiwa Patrick Ayis Ingoi ambaye ni raia wa Kenya.
Ingoi anayetetewa na wakili Fay Sadala alirejeshwa nchini kutokea Kenya Februari 2019, ikiichukua Tanzania miaka 15 kumrejesha nchini, tangu tukio hilo lilipotokea muda mfupi baada ya benki kufungwa saa 9 alasiri ya Mei 21, 2004.
Akimsomea maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Poches Mushi, Ijumaa ya Juni 24, 2022, wakili Kabu alidai siku hiyo, mshitakiwa akiwa na watuhumiwa wenzake, waliingia ndani ya benki hiyo na kujifanya kuwa ni wateja.
Wakiwa ndani ya benki, walijipanga maeneo mbalimbali na baadhi walipanga foleni kuelekea kwa makeshia na walipoanza uvamizi wao baadhi walikwenda hadi ofisini kwa meneja na kuamuru watu wote kulala chini.
Baadaye walipora Sh5.3 bilioni na kabla ya kuondoka, waliwafungia wateja pamoja na wafanyakazi kwenye chumba cha kuhifadhia fedha, huku watu wote wakinyang’anywa simu za mkononi walizokuwa nazo.
ADVERTISEMENT
Kulingana na maelezo hayo, mfanyakazi mmoja wa benki hiyo alifanikiwa kubaki na simu iliyomuwezesha kuwasiliana na makao makuu ya benki hiyo Jijini Dar es Salaam ambao waliwajulisha polisi waliofika eneo la tukio.
Hata hivyo, wakati Polisi wanafika walikuta mshtakiwa na kundi lake walikuwa wametokomea na walipita Jijini Arusha na kujifanya ni watalii na kwenda kutembelea Ngorongoro na Serengeti.
Baadaye mshtakiwa na wenzake walifanikiwa kutoroka nchini kupitia Serengeti hadi alipokamatwa Kenya na Tanzania kufungua maombi ya kutaka arejeshwe nchini.
Mshtakiwa alikanusha maelezo hayo isipokuwa jina lake, anuani yake na kwamba alikamatwa Kenya na kuletwa Tanzania akashtakiwa na kwamba aliwahi kufika Ngorongoro na Serengeti na si kwa uhalifu huo. Kesi itaanza kusikilizwa Julai 6.
Kesi hiyo inasikilizwa wakati raia watano wa Kenya na Askofu wa Kanisa la Christian Fellowship Assemblies of God, Jumanne Kilongola wakitumikia kifungo cha miaka 30 walichohukumiwa Agosti 13,2014 kwa kosa hilo.
Raia hao wa Kenya ni Wilfred Onyango, Patrick Murithi, Gabriel Kariuki, Jimmy Njoroge, Simon Kiambuthi huku mahakama ikiwaachia huru raia watatu wa nchi hiyo, Boniface Mburu, David Mburu na Michael Wathigo kwa kukosekana ushahidi
Mwananchi