Mambo yanazidi kumuendea kombo bondia Hassan Mwakinyo baada ya kuporomka kwa mara nyingine kwenye ubora.
Wiki iliyopita tuliripoti hapa bondia huyo namba moja nchini aliporomoka kwa nafasi 16, kutoka ya 17 hadi 33 duniani kwenye uzani wake wa Super Welter.
Jana ameporomoka tena kwa nafasi mbili hadi nafasi ya 35. Wataapamu wa ndondi wanaeleza kuwa kutocheza muda mrefu ndiko kunamporomosha bondia huyo kwenye ubora.
Mara ya mwisho Mwakinyo anayeishi Florida Marekani kwa sasa, alipigana Septemba mwaka jana na kutetea ubingwa wa Afrika (ABU) kwa Technical Knock Out (TKO) dhidi ya Julius Indongo.
Hata hivyo mwanzoni mwa mwaka huu alivuliwa mkanda huo na ule wa WBF, vyama vyote vikibainisha kuwa amekiuka kanuni zao kwa kutoitetea kwa wakati.
Tangu amewasili Marekani, miezi kadhaa iliyopita Mwakinyo amekuwa akijifua bila kupigana, Inaelezwa kama hatapigana hadi Septemba mwaka huu, mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) utamuondoa kwenye renki kulingana na kanuni zake