Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Lengai Ole Sabaya, baada Wakili upande wa utetezi kuomba kumpeleka hospitali ili akapatiwe matibabu ya uvimbe alionao kichwani.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Salome Mshasha, leo June 7, 2022 Wakili Hellen Mahuna amesema mshitakiwa Sabaya ni mgonjwa na anapaswa kupelekwa Hospitali ili kufanyiwa upasuaji.
“Mshitakiwa namba moja Sabaya ni mgonjwa kutokana na uvimbe uliopo kichwani hivyo tunaomba kesi hii iahirishwe ili akafanyiwe upasuaji,” ameomba Wakili.
ILO yataka uboreshwaji sheria za usalama kazini
Naye Wakili upande wa mashtaka Verediana Mlenzi ameiombia Mahakama kutaja tarehe nyingine ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, kutokana na kutokukamilika kwa upelelezi.
Akijibu hoja hiyo, Hakimu Mshasha ameutaka upande wa mashitaka kuzingatia kauli waliyoitoa Mahakamani Juni Mosi 2022, kuwa upelelezi umekamilika.
Sabaya alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Juni Mosi 2022, kwa mashitaka mapya ya uhujumu uchumi pamoja na wenzake sita, ambayo iliahirishwa kutokana na Hakimu anayeisikiliza kesi hiyo kuwa na majukumu mengine.
Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021 ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 20, 2022.