Mbaroni tuhuma kutumia wanafunzi kufukua kaburi



​​​​​​​JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia Tanga Thadeo (30), mkazi wa Kitongoji cha Kasisiwe, Manispaa ya Sumbawanga, kwa tuhuma za kuwatumia wanafunzi wa Shule ya Msingi Kasisiwe kufukua kaburi la mtoto wake ili amfufue kwa ahadi ya kuwalipa Sh. 10,000.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Theopista Mallya, alisema mtuhumiwa huyo aliwataka wanafunzi hao ambao ni wa darasa la nne na sita wafukue kaburi la mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili kwa kuwa anaamini alifariki dunia katika mazingira ya kishirikina.

Akisimulia kuhusu tukio hilo lililotokea Juni 21 mwaka huu majira ya mchana, Kamanda Mallya alisema siku ya tukio mtuhumiwa alikwenda katika makaburi ya Kasisiwe kwa lengo la kufukua kaburi la mtoto wake, aliyefariki dunia Juni 16 mwaka huu na kuzikwa siku iliyofuata.

Alisema kuwa baada ya mtuhumiwa kufukua kaburi hilo bila mafanikio kutokana na kuchoka, alikwenda kuwaita wanafunzi wa kiume wa shule hiyo waliokuwa wakicheza mpira karibu na makaburi hayo na kukubaliana nao wafukue kwa ahadi ya Sh. 10,000.

Mmoja wa wanafunzi hao ambaye jina linahifadhiwa, alidai kuwa kabla ya kuanza kufukua, mtuhumiwa aliwataka kwanza wasali na aliongoza sala na baada ya hapo walianza kufukua.


 
Alisema baada ya kufukua kwa muda mrefu walilifikia jeneza na ndipo mtuhumiwa alipowaambia waache na aliingia kaburini na kulitoa kisha kulifunga mgongoni kwa kutumia shati alilokuwa amevaa na kuwapa fedha waliyokubaliana awali na kuondoka.

Kamanda Mallya alisema baada ya wananchi kugundua kuwapo kwa kaburi lililofukuliwa na mwili kuchukuliwa, walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa na kituo cha polisi na kufanikiwa kukamatwa mtuhumiwa huyo.

Alisema baada ya mahojiano mtuhumiwa alikiri kulifukua na kuchukua mwili huo kwa madai kuwa alitaka kumfufua kwa sababu haamini kama kifo chake ni cha kawaida, bali ni cha mazingira ya kishirikina.


Kamanda huyo alisema mtuhumiwa ametenda kosa la jinai kwa sababu kama alitaka kufukua kaburi, alipaswa kuomba kibali cha kufanya hivyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad