Mbeya Kwanza ilipanda msimu uliopita na sasa inarudi Championship huku wenzao waliopanda nao, Geita Gold ikitanguliza mguu mmoja kimataifa.
Matokeo ya kupoteza mchezo wao mabao 2-1 Mbeya Kwanza leo dhidi ya Ruvu Shooting imewafanya kushuka daraja na msimu ujao kucheza tena Ligi ya Championship.
Timu hiyo ambayo ilipanda msimu uliopita, ilihitaji ushindi leo ili kuendelea na matumaini ya kubaki Ligi Kuu lakini mambo yamekuwa magumu kwao.
Katika mchezo wa leo uliopigwa uwanja wa Majimaji mjini Songea, wenyeji hawakuonesha soka la ushindani sana na kuwapa nafasi wapinzani kutakata na kujihakikishia kubaki Ligi Kuu kwa pointi 31 wakibaki na mechi moja.
Mabao ya Ruvu Shooting yalifungwa na Full Maganga na Rashid Juma na kuifanya Mbeya Kwanza kubaki na alama zao 24 na mchezo mmoja dhidi ya Simba utakaopigwa Juni 29 mjini Songea.
Mbeya Kwanza hata kama watashinda mechi yao ya mwisho, watafikisha alama 27, ambazo hazitatosha kuwashusha Biashara United walioshinda leo 1-0 dhidi ya KMC na kufikisha pointi 28, huku ikisubiri mwenzake hususani Tanzania Prisons ambao nao hali si hali.
Prisons kwa sasa wako nafasi ya 15 kwa pointi 26, ambapo kesho Jumapili watawakaribisha Simba ikiomba dua ya alama tatu ili kujiweka pazuri kabla ya kumaliza msimu dhidi ya Ruvu Shooting huko mkoani Pwani, Juni 29.
Wakati huohuo, Geita Gold imejihakikishia pia nafasi nne za juu baada ya kuikandika Polisi Tanzania 1-0 na kukusanya alama 45 huku ikitanguliza mguu mmoja kimataifa ikisubiri matokeo ya mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho (ASFC) kati ya Coastal Union dhidi ya Yanga, Julai 2 jijini Arusha.