Dodoma. Mbunge wa Kyela, Ally Jumbe ameeleza kero wanayoipata watu wakati wakisubiri misafara ya viongozi kupita kwenye barabara mbalimbali nchini.
Akichangia bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2022/23 leo Jumatatu Juni 20,2022, Jumbe amesema usalama wa viongozi nchini ni muhimu lakini usalama huo kuna maeneo unawakwaza Watanzania.
“Utakuta kiongozi wetu anasafiri ama anapita sehemu saa tano asubuhi lakini magari yanaanza kufungiwa kupita kuanzia saa 12 asubuhi."
"Spika hili halikubaliki katika teknolojia ya sasa hivi ni nani amewahi kufanya utafiti wa madhara yanayotokea? Mfano mtu alikuwa anaenda mahakamani, halafu akafungiwa mnajua ni watu wangapi wameshindwa kufika mahakamani,” amehoji.
Ameomba watumie njia rahisi ambayo viongozi wanaweza kusafiri hata kwa helkopta akibainisha kuwa kwa sasa Tehama inafika maeneo mbalimbali na kuhoji kwanini hazitolewi taarifa mapema za barabara zinazotumika wakati viongozi wanapita.
“Kama unawahi sehemu uwahi kuondoka. Katika uchumi huu tunaokwenda muda ni muhimu sana tusichezee muda huu,” amesema.
Amesema juzi walikaa kwenye mzunguko (hakuutaja) kwa zaidi ya dakika 40 wakati wanakwenda bungeni lakini baada ya muda huo waliruhusiwa kuendelea na safari bila kiongozi kupita.
“Hii sio nchi ya kujenga uchumi wa blablaa, tujengee uchumi uliokamilika,” amesema.